CCM na Halmashauri ya Jiji la Arusha Kwenye Mgogoro wa Uwanja wa Mpira

0
477
  • Jiji la Arusha laanza kuhoji uhalali wa mali za chama hicho
  • Siri zafichuka kuhusu umiliki Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
  • Ulijengwa kwa nguvu za wananchi na serikali
  • Umiliki wake ulikuwa chini ya Arusha Town Council kabla ya 1996

WAKATI mabadiliko makubwa ya uongozi yakitarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Rais Dk. John Magufuli kukabidhiwa uenyekiti na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, hali si swari kuhusu uhalali wa baadhi ya mali za chama hicho kikongwe nchini.

Ni dhahiri sasa kwamba, Dk. Magufuli, endapo atakabidhiwa uenyekiti, basi ataanza majukumu yake mapya na mgogoro kuhusu mali za chama hicho na mojawapo ya migogoro hiyo ni kuhusu uhalali wa umiliki wa Uwanja wa Michezo wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Uchunguzi wa gazeti hili jijini Arusha umebaini kuwapo kwa mgogoro wa umiliki wa uwanja huo, kati ya CCM na Halmashauri Halmashauri ya Jiji la Arusha, mgogoro unaotiwa nguvu na nyaraka kadhaa.

Uwanja huo wa michezo upo katikati ya mji wa Arusha, kiwanja namba 153 kitalu 21 katika eneo la Kaloleni, ukiwa na ukubwa wa ekari 6.53 na unaweza kuingiza kwa wakati mmoja watu kati ya 16,000 na 20,000, ujenzi wake ukiwa umefanyika kati ya mwaka 1976 na 1977, kwa nguvu za wananchi wa Arusha na serikali.

Taarifa za kiuchunguzi ziizokusanywa na Raia Mwema zinaonyesha kuwa kabla ya uwanja huo kuhamishwa rasmi umiliki wake kwenda CCM, mwaka 1998, ulikuwa chini ya umiliki wa Halmashauri ya Mji wa Arusha (Arusha Town Council).

Historia ya Uwanja
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya watu, wakiwamo baadhi ya wazee wa mji wa Arusha zinaonyesha kuwa eneo lote la uwanja huo, pamoja na eneo yalipo majengo ya CCM lilikuwa linamilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Arusha.

Kwa mujibu wa wazee hao, eneo lote hilo lilikuwa mashamba ya kahawa yaliyomilikiwa na wenyeji ambao waliondolewa na Halmashauri ya Mji wa Arusha kwa malengo ya kupanua maeneo ya mji.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili, mmoja wa wazee walioishi Arusha kwa muda mrefu, Shaban Nyanda, alisema kwa kumbukumbu zake, mwaka 1971 walowezi wawili wa kizungu ambao walikuwa wanajeshi wastaafu wa Jeshi la Uingereza, Kanali Middleton na Kanali Gray, waliomba eneo hilo kwa lengo la kujenga uwanja wa michezo.

“Hawa mabwana walikuwa marafiki wa karibu na ndiyo waliojenga chumba cha kwanza cha X-ray katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru miaka hiyo hiyo ya 1970,”

“Halmashauri ya Mji ilitoa ruhusa kwa ujenzi kufanyika ambapo walowezi hao kwa kushirikiana na wadau wao walijenga ukuta kuzungushia uwanja na kujenga sehemu ya kuchezea (pitch) na pia viwanja vidogo vinne kwa ajili ya michezo mingine kama mpira wa wavu, mpira wa kikapu na mpira wa netball,” alisema mzee Nyanda.
Mzee huyo alisema ujenzi wa uwanja huo ulianza mwaka 1971 na kukamilika mwaka 1972 na ulitumika hasa kwa mchezo wa soka uliokuwa ukipendwa sana na wazungu hao wawili. Uwanja huo ulijulikana kama King George V1 Stadium.

“Mwaka moja baada ya ujenzi kukamiliki Kanali Middleton na mwenzake Gray alikabidhi uwanja huo kwa Halmashauri ya Mji wa Arusha na kwa heshima yao barabara inayotoka Mianzini kuingia Kituo Kikuu cha Mabasi inayopita pembezoni wa uwanja ilipewa jina lake ambalo limedumu hadi leo,”
“Historia ya uwanja huo ilibadilika kati ya mwaka 1976/1977 baada ya serikali kuamua uvunjwe na kujengwa upya na kupewa jina kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta ambaye alikuwa mmoja wa wanasiasa na magwiji wa lugha ya Kiswahili hapa nchini,”alisema.

“Nakumbuka wakati wa ujenzi, wananchi tulichangia fedha na nguvu zetu, kila aliyepita kwa shughuli zake jirani na uwanja wakati ujenzi unaendelea alikamatwa kwa nguvu afanye kazi kwa kujitolea. Tulibeba matofali kwa vichwa…ilikuwa kazi kweli kweli,” anaongeza mzee mwingine, Mrisho Hamis Mayunga, maarufu kwa jina la mzee Pigabao.

CCM wautwaa kinyemela
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Raia Mwema imezipata, hati ya umiliki wa uwanja ilibadilishwa rasmi mwaka 1998 kutoka kuwa wa halmashauri na kupewa CCM.

Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa tangu ujenzi wa pili ufanyike mwaka 1976/1977, hakuna mapato ya uwanja huo ambayo yamewahi kuwasilishwa kwa halmashauri ya mji kutokana na kile kinachoelezwa ubabe wa viongozi wa CCM, wakitumia turufu ya chama kushika hatamu.

Aidha taarifa zaidi zinaeleza kuwa katika kipindi chote hicho, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ambao wote walitokana na chama hicho, walipinga kitendo hicho ingawa walishindwa kujitokeza hadharani kwa hofu ya kuadhibiwa na chama.

Uthibitisho na dhana kuwa uwanja huo ulikuwa mali ya Halmashauri ya Mji uko katika barua ya Januari 4, mwaka 1986, iliyoandikwa na Mohamed Lusenna kwa niaba ya Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha yenye kichwa habari “UMILIKAJI WA UWANJA WA MICHEZO WA SHEIKH AMRI ABEID”.

Katika barua hiyo, Lusenna ambaye ni ofisa wa CCM ngazi za juu Mkoa wa Arusha anawaagiza watendaji wa halmashauri akiwemo Mkurugenzi, Ofisa Maendeleo ya Ardhi na Jamii na Ofisa Mipango kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, kujadili umiliki wa uwanja huo.

Hata hivyo taarifa zinabainisha kuwa katika mazungumzo hayo, mwafaka haukuweza kupatikana baada ya maafisa wa Halmashauri ya Mji wakati huo kushauri kuwa suala hilo lipelekwe kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani.

CCM iliendelea na harakati zake za kuutwaa uwanja huo ambapo mwaka 1989, Ofisa Maendeleo ya Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Arusha, E.K.E.Makere alimwandikia barua Ofisa Maendeleo ya Ardhi Mkoa akitaka ufafanuzi kutokana na hatua ya CCM kutaka wapewe hati miliki ya uwanja huo.

Barua hiyo yenye kumbukumbu namba AR/3871/1/EKEM ya Mei 16 mwaka huo inaeleza: “Siku za nyuma kiwanja hiki kilijulikana kama King George V1 Memorial Stadium na kwa utaratibu viwanja vingi vya michezo viko chini ya Halmashauri za Miji, Manispaa au Jiji”.

Anaendelea katika barua hiyo: “Kiwanja hiki kilijengwa upya miaka ya 1976/1977 kwa usimamizi wa chama na sasa hivi wanataka hati ya kuumiliki kwa maelezo hayo, naomba maelekezo ni mamlaka gani hasa iliyo na haki ya kumiliki kiwanja hicho”.

Barua hiyo inahitimishwa kwa kusisitiza: “Nadhani utazingatia umiliki wa miaka ya nyuma kabla kiwanja hicho hakijajengwa upya na hali halisi ya wakati huu.”

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa CCM na uongozi wa Halmashauri ya Mji waliendelea kuvutana kuhusu uhamishaji wa hati hiyo ambapo katika kikao cha Oktoba 16 kati ya viongozi wa chama hicho Mkoa na Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Mji, walikubaliana kuwa wajadiliane kuangalia uwezekano wa CCM kuilipa fidia Halmashauri ya Mji.

Katika dokezo lake (memo) kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Ofisa Maendeleo ya Ardhi J.M. Chaula, Oktoba 23, anabainisha kuwa Kamati ya Siasa ya Mkoa na Kamati ya Fedha zikutane kujadili namna gani manispaa inadai kulipwa fidia kiasi gani.

Agosti 20, mwaka 1996, Ofisa Ardhi wa Mkoa wa Arusha, P.H.Muhale kwa barua yenye kumbukumbu namba AR/3879/10 alimwandikia Ofisa Maendeleo ya Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha kuwa ameagizwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha kufanya upimaji wa uwanja ili hatua za kutoa hatimiliki kwa CCM ziweze kufanyika.

Sehemu ya barua hiyo inasomeka: “Nimeagizwa na Mkuu wa Mkoa nifanye kazi ya upimaji wa kiwanja hicho ili hatua za kutoa hatimiliki kwa CCM iweze kuchukuliwa”.

Katika barua hiyo Muhale anahoji: “Tafadhali nifahamishe kama upimaji wa kiwanja hicho uliwahi kufanywa na halmashauri, na kama ndiyo ulikamilika na kusajiliwa? Je, kuna utata nani amilikishwe kiwanja hicho?

Taarifa zinaoonyesha kuwa wakati huo Mkuu wa Mkoa alikuwa Daniel ole Njoolay ambaye aliteuliwa kushika wadhifa baada ya Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais, Benjamin Mkapa, kuingia madarakani mwaka 1995 katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.

Umiliki ulivyohamishwa CCM
Taarifa zinaonyesha tangu kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Arusha mwaka 1996, Njoolay alishinikiza kwa maofisa wa Manispaa ya Arusha kuwa wakabidhi uwanja huo kwa CCM haraka na kusaini nyaraka zilizokuwa zinahitajika bila Baraza la Madiwani kushirikishwa.

Hata hivyo, juhudi za gazeti hili kumpata ole Njoolay kuzungumzia husika wake katika uhamishaji huo hazikuweza kufanikiwa kwa siku tatu mwishoni mwaka wiki hii.

Habari zaidi za uchunguzi zinaonyesha kuwa umiliki wa uwanja huo ulihamishwa kwenda CCM mwaka 1998 na kupewa hatimiliki namba 14216 iliyotolewa Oktoba 28 mwaka huo na Kamishna wa Ardhi mjini Moshi, ikiwa na hati (lease) ya miaka 33.

Raia Mwema inazo taarifa za uhakika kuwa wakati umiliki huo unahamishiwa kwenda CCM na baada ya mchakato kufikia ukingoni hati ya awali iliyokuwa ikimilikiwa na Halmashauri ya Mji ilifutwa na nyaraka nyingi ziliteketezwa kwa malengo ya kuondoa ushahidi na ufuatiliaji.

“Hatua ya ole Njoolay kushikiana na maofisa wa manispaa bila kuwashirikisha wajumbe wa Baraza la Madiwani ambacho ni chombo cha juu kabisa cha kufanya uamuzi wa halmashauri ilikuwa ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uendeshaji wa shughuli za serikali,” anaeleza Mwanasheria James Lyatuu.

Aidha pia uhamishaji wa hatimiliki huo ulifanyika wakati tayari Tanzania ilikuwa katika mfumo wa vyama vingi hivyo haikupaswa mali ya umma kutwaliwa na chama kimoja cha siasa wakati awali, mali hiyo ilikuwa ya umma kwa mujibu wa mwanasheria huyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ungalimited (Chadema).

Ikumbukwe kuwa mchakato wa kuanzishwa kwa vyama vingi ulianza mwaka 1992 na hadi kufikia mwaka 1994, Serikali ya Awamu ya Pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi iliridhia kuanzishwa kwa mfumo huo na uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka 1995.

“Walichofanya CCM ni ukiukwaji mkubwa wa kupora mojawapo ya vyanzo muhimu vya mapato kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kutokana na msingi kuwa uwanja huo unazalisha mapato mengi kutokana na shughuli mbalimbali za michezo, matamasha ya muziki, mikutano ya kisiasa pamoja na ile ya dini”, aliongeza Lyatuu.

Takwimu zinaonyesha kuwa uwanja huo kwa nje umezungukwa na maduka 60 ambayo yote hulipa wastani wa shilingi 400,000 kwa mwezi kama kodi ya pango kwa CCM.

Kwa hesabu hizo, kwa kodi ya pango pekee wakadiriaji wa mahesabu wanakadiria kuwa chama hicho huingiza kiasi cha shilingi milioni 24 kwa kodi ya pango pekee sawa na sawa na wastani wa milioni 288,000,000 kwa mwaka na kwa miaka 18 tangu walipopata hati miliki chama hicho kilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 10.

Hesabu hizo za kodi ya pango ni tofauti na mapato ya michezo mbalimbali ya soka ikiwemo mechi kubwa za klabu maarufu za Yanga na Simba ambao huingiza mapato ya mamilioni ya shilingi zinapocheza Arusha, matamasha ya muziki, mikutano ya kisiasa na ile dini ambayo yote hulipa wastani wa shilingi milioni 2,000,000 hadi 5,000,000 kulingana na uzito wa shughuli.

Wakadiriaji wa hesabu wanaeleza kuwa katika kipindi cha miaka 30 ambayo chama hicho kilihodhi uwanja huo na kujichukulia mamlaka ya kukusanya mapato kilipata mabilioni ya fedha yanayokadiriwa kufikia mabilioni ya shilingi.

Kwa mujibu wa mtaalamu mmoja wa Jiji la Arusha kutoka ofisi ya mweka hazina, fedha hizo zingekuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya jiji kwa msingi kuwa zingetumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta nyeti kama elimu, maji, afya na miundombinu.
“Kwa mabilioni hayo unaweza ukajenga kilomita 100 za barabara za lami ndani ya jiji, shule za msingi na sekondari za kutosha vituo na zahanati karibu katika kata zote 25 na hata katika mitaa 150, hizi ni fedha nyingi sana”anaeleza mtaalamu huyo ambaye jina lake linahifadhiwa.

Kauli za viongozi
Kwa upande wao, uongozi wa CCM Mkoa wa Arusha haukuwa tayari kuzungumzia suala wakieleza kuwa kushangazwa na gazeti hili kutaka “kufukua makaburi”.

“Nawashangaa Raia Mwema tunawaheshimu sana kwanini mnajaribu “kufukua makaburi” ya zamani? Ili mpate nini? Mimi siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu ni mambo yaliyofanyika miaka 17 iliyopita,” alisema kiongozi huyo ambaye aliomba asitajwe gazetini.
Meya wa Jiji la Arusha Kalist Lazaro (Chadema) aliiambia Raia Mwema kuwa wanafahamu suala hilo tangu walipoingia madarakani mwanzoni mwa mwaka huu na kudai kuwa kilichofanyika ni “wizi” wa mchana wa mali ya umma.

“Tunazo hizo taarifa na tunaamini kwamba ni wizi wa mali ya umma kwa sababu utaratibu wa kuhamisha umiliki ni batili. Mkuu wa Mkoa ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa hana mamlaka yoyote kuhusu mali za halmashauri hivyo kilichofanyika ni uhamishaji mali haramu,” alisema Meya huyo na kuongeza; “Kwa sasa suala hili linaangukia katika mkondo wa kisheria na utawala tunamwomba Rais John Magufuli atumie busara zake kwa kuwa hili liko chini ya mamlaka yake kwa kufuta hati hiyo ili uwanja huo urudi mikononi mwa umma”.

Lazaro aliongeza kuwa hata hivyo watafanya kila wawezelo kutumia njia za kidiplomasia ili uwanja huo urudi mikononi mwa Halmashauri ya Jiji kwa kuwa eneo hilo ni moja ya kitega uchumi na chanzo cha mapato muhimu kwa jiji lake.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa lawamani kwa kuhodhi mali kama majengo, viwanja, mashamba viwanja vya michezo katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini ambayo mengi yalikuwa yanamilikiwa na taasisi za umma na kuhamishia umiliki wake kwa chama hicho baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.

Chanzo raia mwema

Leave your comment about CCM na Halmashauri ya Jiji la Arusha Kwenye Mgogoro wa Uwanja wa Mpira using the comment form below

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here