Hotuba ya Prof Sospeter Muhongo akitangaza nia ya kuwania Urais (CCM)

0
1240
Professor Sospeter Muhongo Atangaza Nia Urais 2015 Kupitia CCM

Mbio za wanachama ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza nia ya kutaka Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho zimezidi kushika kasi ambapo aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo ametangaza nia akiwa mkoani Mara kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu Huria Musoma.

Hapa tumekuwekea sehemu ya hotuba aliyoitoa akijaribu kufafanua na kueleza kwa nini anautaka Urais wa Tanzania.

Niko mbele yenu sio kufanya kampeni ya urais, niko mbele yenu kuomba ridhaa ya yenu kugombea nafasi ya urais muda ukifika. Siko hapa kumlaumu mtu au kumshambulia mtu, kwa sababu ukimlaumu mtu umasikini bado uko palepale.

Nikisema historia yangu yote muda hautatosha. Kisomo nimesoma mpaka mwisho wa kusoma, kama ni taaluma nimefikia mwisho. Nimepata bahati ya kusoma vyuo vikubwa sana duniani na sehemu kubwa nimepatia Ujerumani ndio maana wengine wanasema nafanya kazi kijerumani.

Nimefanya utafiti kwa miaka 30, chama cha majiologia wa Marekani kilichoanza mwaka 1988, mimi niko ngazi ya juu. Pia kwa waingereza na wachina niko ngazi ya juu kabisa.

Kwenye uasisi mwaka 1976, CCM inaanza 77 sisi ndo waasisi, kadi hii hapa. Kama nimeweza kutunza kadi ya CCM tangu 75 basi mimi ndio naweza kutunza rasilimali zenu.

Toka tunapata uhuru tuna vikwazo, ujinga, maradhi na umasikini Mwl alitueleza. Ni lazima matatizo yatakuwepo kwenye jamii.

Rushwa kubwa na ndogo, ukosefu wa ajira, siasa imekwenda kila mahala, taifa linanyemelewa na uvivu na utegemezi, dhulma, upungufu wa upatikanaji wa takwimu sahihi, tumepungukiwa ushindani kama taifa, tumeshindwa kujiamini. Haya ndio nataka kuyashughulikia mimi.

Upungufu wa mshikamano wa taifa letu. Kwetu asilimia 51 waislamu na 49 wakristo hivyo matatizo ya madhehebu hapa ndipo mahala pake. Afrika ina nchi 54, mimi nimeeenda 52 kasoro Mauritania na Chad. Ningekua sio muaminifu nisingepokelewa huko, ulaya nimezunguka.

Lazima tujue hali halisi ya uchumi wetu, chukueni kalamu na karatasi. Lazima useme unatoka wapi unaenda wapi! India asilimia 74 wanajua kusoma na kuandika. Nchi inayoongoza kwa watafiti ni Finland.

Anataja takwimu za nchi ambazo tulikuwa tunafanana uchumi baada ya vita ya pili ya dunia ikiwemo India, Brazil, China na Kenya. Sipendi sana kujilinganisha na Kenya kwa sababu sote ni maskini.

Anaendelea…

Dira ya maendeleo inasema miaka kumi kutoka sasa Tanzania isiwe nchi masikini, tusikae pembeni, tusogee juu kidogo. Hakuna mwenye uwezo huo ni mimi tu ili tufikie pato la dola bilioni 200 kutoka dola bilioni 40. Mwaka 2025 tutakuwa milioni 60, nataka tule mihogo na viazi kwa hamu na sio kwa shida.

Siwezi kukupa ahadi ya mishahara wakati sijakuza uchumi, siwezi kukupa ahadi ya kukujengea shule wakati sijakuza uchumi, tukuze kwanza uchumi.

Naombeni ridhaa yenu nisimamishe deni la taifa lisiongezeke, mwenye dawa ya umaskini ndani ya CCM, CHADEMA, NCCR ni profesa Muhongo tu. Elimu kuiboresha lazima tuongeze bajeti, haiwezekani darasa limerundikana ukafundisha.

Anaeweza ni mimi tu sababu wengine utafiti wanausoma kwenye magazeti tu.

Wana CCM mnae mwanasayansi wa dunia, si mnipe tu! Tutatumia rasilimali, madini yetu tumeyachimba kwa asilimia 10 kitu. Mimi ndio nimetengeneza ramani ya madini ya Tanzania, Africa na duniani nikiwa vice president. Nilizunguka hii nchi kuchora ramani ya madini kwa uzalendo, ningeweza kuja na ramani na kuiuzia serikali.

Mimi mtu hanidanganyi, unakuja tunajadiliana, hii sio dunia ya kuandikiwa tu, inabidi na wewe ujiandikie. Niliweka mipango ya kuwapunguzia bei ya umeme. Ilibidi nitoke kidogo mpate machungu mnichague. Nawaomba ifike mahala ifike mahala tuachane na matumizi ya kuni na mkaa, ni aibu sana. Tutajenga mabomba nchi nzima gesi itumike majumbani. Kila nyumba iwe na mabomba mawili, la maji na la gesi.

Wengine mnaweza kuwadanganya, mimi hamuwezi kunidanganya, gesi yenu ipo kwenye mikono ya uhakika kwa Profesa Muhongo tangu nimeanza kusoma wakati niko chuo kikuu cha Dar es Salaam na nimefanya maisha yangu yote.

Mapato ya gesi yasiende hazina, tutafungua mfuko maalumu na bunge litakua linaidhinisha asilimia ngapi iende kwenye bajeti. Mtanzania yoyote asiwe na maamuzi ya kutumia hizo fedha bila idhini ya watanzania.

Mimi sipendi wawekezaji wababaishaji na si kwamba sipendi wawekezaji wa ndani, haya yote ya ujenzi wa uchumi lazima tuwe na umeme. Na umeme wa bei nafuu ndio kazi niliyokuwa naianza. Umeme ulikuwa haukatiki mara kwa mara, muda umefika tusijidharau, lazima tushinde.

Lazima watanzania zaidi ya asilimia zaidi ya 75 wawe wanatumia umeme, tutatumia vyanzo vyote vya umeme. Lazima mtembee kifua mbele professa Muhongo ametimiza ahadi ya CCM, hata ilani mpya inayokuja mtekelezaji atakaetekeleza kwa uhakika ni Profesa.

Ni lazima tupambane na rushwa, na sio maneno kupambana nazo na nyie wananchi muwe na uelewa na haki zetu. Mnaombwa rushwa kwa sababu hamjui haki zenu. Naomba ridhaa yenu mniteue niwe mgombea wenu. Wakulima na wafugaji ni mwisho wa kuuana chini ya Prof. Muhongo, tatizo sio ardhi, ni teknolojia.

Uwezo ninao, maarifa ninayo, jinsi ya kutafuta fedha ndani na nje, ambacho sina ni nyinyi kuniteua tu.

 

Acha maoni yako kuhusu kwa kutumia fomu hapa chini

Weka majibu hapa

Tafadhali weka maoni
Tafadhali weka majina yako hapa