Edward Ngoyayi Lowasa: Mchapa kazi mwenye nakisi ya uadilifu na falsafa
Na Profesa Kitila Mkumbo
Katika makala mbili nilizoandika na kuchapishwa katika gazeti hili wiki mbili zilizopita nilijaribu kuanisha sifa za kihaiba na kikazi za mwananchi anayefaa kuwa Rais wetu wa tano. Nashukuru kwa mrejesho niliopokea kutoka kwa wasomaji wengi na walionitia shime niendelee na makala hizi.
Nawashukuru pia waandishi wenzangu wa makala, akiwemo mwandishi mahiri na mkongwe, Johnson Mbwambo, kwa kurejea maudhui ya makala yangu katika andiko lake lililochapishwa katika gazeti hili toleo Na. 370 la Septemba 10-16, 2014. Nakubaliana kwa kiasi kikubwa na hofu aliyoonyesha juu ya uwezekano wa wagombea kukidhi sifa nilizozianisha, pamoja na hitimisho lake kwamba wagombea waliokwishajitokeza hadi sasa wana ombwe kubwa la kifalsafa.
Nilisitisha kwa muda makala hizi kutokana na uzito wa maoni niliyopokea kutoka kwa watu mbalimbali, wakiwemo viongozi waliojijengea heshima kubwa katika nchi yetu. Wengi wa waliotoa maoni walienda mbali na kunishauri niandike kitabu kuhusu wasifu wa wagombea.
Wengine waligutuka nilipohitimisha makala yangu kwa ahadi ya kuanza kuwajadili wagombea moja baada ya mwingine, wakidhani kwamba nitakuwa nakwenda mbali mno! Aidha, wapambe wa wagombea nao wamekuwa na wasiwasi kwamba nitawabeba baadhi ya wagombea na kuwaharibia wagombea wao. Baadhi ya wasomaji na wapambe wa wagombea wamenishauri kwamba niache kuwajadili wagombea na niwaachie wananchi waamue wenyewe. Nimekataa ushauri wao huu wa kuwachia wananchi waamue wenyewe, na hivyo naendelea na uchambuzi wangu wa wagombea wote waliojitokeza na watakaojitokeza.
Nimeamua kujitwika jukumu hili hatarishi kama sehemu ya wajibu wangu wa kijamii katika kuchangia kuiepusha nchi kupata kiongozi atakayetushtukiza bila kumjua sawasawa kabla hajaingia madarakani. Ukimwacha Mwalimu Nyerere, marais wetu waliopita na aliyepo walitushtukiza. Hatukumjua vizuri Mzee Mwinyi kabla hajawa Rais, na vivyo hivyo kwa Mzee Mkapa. Wote hawa walipatikana kwa mtindo unaofanana: waliibuliwa bila kujitutumua wao wenyewe kuutaka urais kwa udi na uvumba kama ilivyo kwa wagombea wa leo. Mzee Mwinyi aliibuliwa na Kamati Kuu ya CCM, wakati Mzee Mkapa aliibuliwa na Mwalimu Nyerere pasipokutarajiwa. Bahati nzuri waliibuliwa katika mtindo usiotia shaka sana kwa sababu ni uzao wa taasisi za kueleweka kwa wakti ule, ambazo ni Mwalimu mwenyewe na Kamati Kuu ya CCM ya wakati huo ambayo isingekuwa rahisi kuitilia shaka katika maamuzi yake.
Pengine tulimjua kidogo Rais Kikwete kabla ya kuingia madarakani kwa sababu alijinadi vya kutosha kabla hajaingia ikulu mwaka 2005. Jina la Rais Kikwete lilianza kuwika kwa upana wake kwa mara ya kwanza mwaka 1995 alipochukua na kurudisha fomu ya kugombea urais kwa mbwembwe, sambamba na sahibu wake mkuu wa wakati huo Ndugu Edward Lowasa. Tangu wakati huo tuliendelea kumwagiwa sifa kemukemu juu ya Rais Kikwete hadi anaingia madarakani mwaka 2005. Kwa hiyo, hatukujua upande wa pili wa Rais Kikwete kwa maana ya udhaifu wake kihaiba na kiutendaji kabla hajaingia madarakani. Ndiyo kusema naye kwa kiasi fulani alitushtukiza.
Yote hii ni kwa sababu tumekuwa hatuna utamaduni wa kuwadodosa vya kutosha watu wanaotaka kuwa viongozi wetu. Maandishi mengi kuwahusu wagombea huandikwa wakati wa kampeni yakilenga kuwasifu wagombea fulani na ‘kuwakandia’ wagombea wengine. Hatupati uchambuzi unaotuwezesha kuwajua wagombea wote kwa ukamilifu wake katika kutusaidia kufanya maamuzi ya maana. Hili ndilo ombwe la ufahamu ambalo najaribu kuliziba katika mfululizo wa makala zangu.
Katika uchambuzi wangu nitajitahidi kuwa mkweli na kuzingatia maadili na weledi wa kitaaluma ili kuepuka kupendelea au kuonea. Hata hivyo, kama yalivyo maandishi yote katika sayansi ya jamii, sitarajii kwamba makala hizi hazitaibua hisia kali, shutuma, lawama na hata vitisho kutoka kwa miongoni mwa wapambe wa wagombea ambao wamejiaminisha kwamba wagombea wao ndio hasa wanaofaa kuongoza nchi hii na hakuna mwingine.
Niwatahadharishe wasomaji na hasa wapambe wa wagombea kwamba ninachokiandika hapa ni wasifu wa wagombea, kwa maana ya “biography” na sio wasifu kwa maana ya “hagiography”. Katika kuandika hagiography, mwandishi hujikita katika kuanisha mazuri ya mtu anayemwandika huku akifumbia macho madhaifu au mapungufu yake. Katika kuandika biography mwandishi hujikita katika kuanisha pande mbili za mhusika ikiwa ni mazuri na mapungufu yake.
Kimsingi hagiography huandikwa kwa ajili ya kuwatukuza na kuwasifu ‘watakatifu’ wanaoishi. Bahati mbaya au nzuri hatuna hata mtakatifu mmoja kati ya wagombea wetu. Hivyo, tutachambua nguvu na mazuri yao kwa upande mmoja, na madhaifu na mapungufu yao kwa upande mwingine. Ni matumaini yangu kwamba uchambuzi huu utawasaidia wagombea na wapambe wao katika kujiimarisha kwa kukazia nguvu na mazuri yao na kuchukua hatua stahiki katika kurekebisha au kujiandaa kujibu mapigo kuhusu madhaifu na mapungufu yatakayojitokeza katika makala hizi.
Tunaanza na Ndugu Edward Ngoyai Lowasa. Huyu alipata kuwa waziri mkuu katika awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Kikwete aliyedumu kwa takribani miaka mitatu kutoka 2005 hadi 2008.
Ndugu Lowasa ndiye mwanasiasa pekee mwenye uwezekano wa kugombea tena urais kati ya wanachama 17 wa CCM waliojitokeza kugombea urais mwaka 1995. Wengine waliobaki ama wamefariki dunia (wakiwemo Horace Kolimba, Tuntemeke Sanga, Kigoma Malima), au wamezeeka na kuishiwa nguvu za kukabiliana na mikiki ya kisiasa (wakiwemo John Malecela, Cleopa Msuya, Pius Msekwa, Joseph Warioba), au ‘wamepotea’ katika ulingo wa siasa (wakiwemo Rose Lugembe, Solomon Ole Saibul, Aggrey Mwasagah, Omari Mwariko, Balozi Frederick Rutakyamirwa).
Wana CCM wawili kati ya wale waliojitokeza mwaka 1995 walifanikiwa kuukwaa urais katika vipindi tofauti, ambao ni Mzee Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete (2005-2015). Mzee Mark Bomani aliyegombea pia mwaka 1995 naye bado yumo katika ulingo wa siasa lakini hajaweka wazi kama atagombea au la hadi ninapoandika makala haya, lakini kuna watu kadhaa wanamtajataja.
Edward Lowasa alijitokeza mwaka 1995 akiwa na mika 42 tu mbele kidogo ya January Makamba (miaka 40), ambaye naye amejitokeza kugombea akitembelea kete ya ujana. Aidha, pamoja na kwamba hajawahi kutangaza rasmi na moja kwa moja, Ndugu Ngoyai Lowasa ni mwanasiasa ambaye anatajwa kwa uhakika zaidi kwamba anautaka urais 2015, na pengine amejiandaa zaidi kisaikolojia kuwa Rais kuliko mgombea mwingine. Kwa hivyo, Ndugu Lowasa ni moja ya wagombea wenye nguvu za kisiasa za kuweza kushinda uteuzi ndani ya CCM na pengine kushinda kiti cha urais.
Kikazi, Ndugu Edward Ngoyai Ngoyai Lowasa ni mwanasiasa ambaye tunaweza kumuelezea kama kiongozi anayebebwa na taswira chanya ya uchapa kazi katika sehemu mbalimbali alizofanya kazi, ikiwemo alipokuwa waziri mkuu. Kihaiba, Ndugu Lowasa anazungukwa na taswira hasi katika eneo la uadilifu, kutokana na kuhusishwa na tuhuma na hisia nyingi kuhusu rushwa na ufisadi hapa nchini. Pengine hiki ndicho kitakuwa kikwazo kikubwa zaidi katika mbio zake za urais kwa sababu uadilifu itakuwa moja ya agenda kubwa katika kampeni za 2015. Akifanikiwa kupenya uteuzi wa CCM atakuwa na kazi ya kutosha kujibu maswali mengi kuhusu tuhuma za ufisadi. Tutachambua taswira hizi pamoja na sifa zingine za Ndugu Lowasa katika makala ijayo.