LOWASSA KAFARA CCM KUJARIBU KUZUIA MABADILIKO

2
1863
Edward Ngoyai Lowassa Akitafuta wadhamini wa Urais 2015

Na Ananilea Nkya

Nimeandika  hoja hii baada ya kusoma na kusikia  hoja zinazotolewa na  baadhi ya Watanzania kwamba  eti CHADEMA , CUF, NCCR-Mageuzi  na NLD  -vyama vinavyounda UKAWA kwa kumsimamisha   Edward Lowassa kugombea Urais  vimepoteza usafi  wa kuongoza  mapambano dhidi ya ufisadi.

Ukweli ni kwamba viongozi wa CHADEMA na UKAWA kumsimamisha Lowassa kuwa mgombea urais wamecheza kama Pele. Tena wanastahili pongeze kubwa maana walitumia akili kali na saikolojia ya hali ya juu kubaini kuwa CCM ilikuwa ilicheza mchezo mchafu kisiasa kuwatumia wapinzania kumpakazia Lowassa ufisadi na hatimaye CCM kupata nguvu ya kumtoa Lowassa kafara ili eti CCM ionekane inajisafisha ufisadi.

Wanaodhani CHADEMA na UKAWA wamekosea pengine hawajaelewa kuwa   tangu upepo wa mabadiliko  wa kukataliwa mfumo chama kimoja kuwa madarakani kwa muda mrefu ulipoanza kuvuma duniani kote mwishoni mwa miaka ya 1980,  baadhi ya wanaCCM hawajakubali kwa dhati kabisa  ukweli huo na kuamini kwamba  CCM inaweza  kupunzishwa kuongoza nchi angalao kwa miaka mitano.

Hasa baada ya Mwalimu Nyerere CCM kuondoka duniani, CCM imebaki na viongozi ambao hawako tayari kutumia ujasiri kuongoza mabadiliko kwa amani.  Baadhi ya vongozi wanaojali zaidi maslahi ya wana CCM wachache wanaotumia kauli kama hirizi kauli aliyowahi kuitoa Mwalimu Nyerere kuwa bila CCM imara—Tanzania itayumba kujidanganya wenyewe na kudanganya wananchi.

Wanasahau kwamba Mwalimu Nyerere kama mwanafalsafa na mwanasiasa makini alikuwa anatoa maamuzi ya kijasiri kwa faida ya taifa na wananchi kulingana na hali halisi ya wakati husika kwa kusoma upepo wa wananchi. Kwa mfano Nyerere aliwahi kusema CCM si mama yake akimaanisha Tanzania na Watanzania ni muhimu zaidi kuliko umuhimu wa CCM kuwa madarakani.

Mfano Mwalimu Nyerere mwaka 1992 alionyesha mfano kwamba maslahi ya nchi na wananchi ndiyo muhimu kuliko maslahi ya CCM alipokubali kwenda kinyume na uamuzi wa wanaCCM wengi waliokuwa wamekataaa—mabadiliko—kuanzishwa vyama vingi nchini ili vyama vibadilishane uongozi wa nchi –kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Lakini baada ya Mwalimu kuondoka dunaini kila mwanaCCM anayechaguliwa kuwa Rais, kwa kuogopa kulaumiwa kwamba eti kama CCM haitachaguliwa kupitia sanduku huru la kura atabeba lawama za kufanya CCM iondoke madarakani, serikali zote za CCM baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka duaniani zimekuwa zinajihusisha na ufisadi.

Serikali ya CCM imekuwa ikikwapua kwa wizi wa wazi mabilioni ya fedha za umma na kufanya maovu mengine mengi kuhakikisha CCM haiondoki madarakani. Hivyo chaguzi zinafanyika kama geresha tu—kudanganya wafadhili na mataifa kuwa Tanzania ni nchi ya demokrasia ya vyama vingi.

Mfano uchaguzi wa mwaka 2005 serikali ya CCM chini ya Rais Mkapa ilikwapua fedha za wananchi kutoka Benki Kuu Akaunti ya EPA shilling bilioni 133 ambazo ziliiwezesha CCM kumweka madarakani Rais Kikwete.

Mwaka jana 2014 serikali ya CCM chini ya Kikwete ilikwapua shilingi bilioni 306 kutoka akaunti ya Tegeta escrow Benki Kuu kwa ajili ya kuiwezesha CCM kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015.

CCM wakishaingia madarakani jambo muhimu kuliko yote Rais na serikali yake analolifanyia ni kubuni ufisadi wa kuipatia CCM fedha na mbinu nyingine za kuiwezesha CCM ibaki madarakani uchaguzi unaofuta. Hakuna kazi muhimu ya kuwaondolea wananchi umaskini inayofanyika kwa kiwango na juhudi kubwa.

Kwa sababu hiyo,   kikundi kidogo cha watawala, wengi wakiwa ni kutoka CCM na familia zao wamejikuta wakinufaika kwa kuwa  matajiri kufuru kwa muda mfupi ili hali  wananchi wengi wakibaki maskini na mafukara wa kutupa.

Mfano  wabunge (kikundi cha watu wasiozidi 400) wengi wakiwa  ni wanachama wa CCM  kila mmoja analipwa si chini ya milioni  10 kila mwezi kama mishahara, wacha marupurupu  na posho za vikao vya kamati, posho za safari na  mamilioni mafao kila baada ya miaka mitano.  Lengo wawe na fedha nyingi za kununua kura za wapiga kura maskini uchaguzi unaofuata CCM ibaki madarakani.

Ndiyo sababu kila mwananchi wakiwepo watu muhimu kama walimu wa vyuo vikukuu na madaktari hivi sasa nao  wameamua kuwa wanasiasa.

Zaidi baadhi ya wanaotafuta madaraka ya kisiasa wanatumia mbinu chafu sana  ikiwa ni pamoja na ushirikina wa kuuwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) waweze kupata nafasi ya kuingia katika kundi la  watawala—kupata utajiri wa kutisha katika kipindi cha miaka mitano.

Mfamo Wabunge waliomaliza muda wao mwaka huu 2015    kila mmoja ameondoka na kiinua mgongo zaidi ya shilingi milioni 200.  Hii ni kufuru katika nchi inayojinasibu kuwa ni maskini na inapita huko na huko duniani kuomba misaada!

Hata hivyo kwa kadri ufukara unavyoendelea kuwatafuna wananchi wengi, na kwa kadri uelewa wa  wananchi  wanaoteseka kwa  umaskini  unavyoongezeka kwamba CCM na utawala wa  serikali yake ndicho chanzo cha umaskini wao,  CCM  imebaini kuwa haiwezi tena  kushinda uchaguzi kupitia sanduku huru la kura kwa kutegemea kete moja tu—kununua wananchi mafukara  peke yake.

Hivyo katika miaka ya hivi karibuni CCM imeanza kuendesha siasa za maji taka—kuchafuana wao kwa wao na hatimaye wameamua kutoana kafara-lengo kuu likiwa ni kuzuia wananchi wasitumie sandundu la kura kufanya mabadiliko—kuchagua vyama vingine kuongoza nchi.

Hivyo Rais Kikwete, hata kama ndani ya umungu wa moyo wake hakubaliani na CCM inavyotumia ubabe kukataa mabadiliko kinyume na asili ya binadamu, amekuwa akifanya mambo kutimiza matakwa ya baadhi ya wanaCCM —kujaribu kuzuia mabadiliko—ili tu kuepuka lawama- amalize muda wake bila kuonekana ndiye kasababisha wananchi kuipunzisha CCM uongozi kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa kufanya hivyo Rais Kikwete amejikuta akiporwa ujasiri wake aliokuwa nao kama mwanasiasa   ambaye Mwalimu Nyerere alimuamini.

Kumbuka Mwalimu Nyerere alinukuliwa na gazeti la  Nipashe na Majira 26/5/95 akisema   baada ya Rais Mwinyi  baadhi ya vijana ambao alikuwa anaona wana nia ya dhati kabisa  na uwezo mkubwa wa kuongoza Tanzania  ni Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa.
Lakini kwa Kikwete kukubali kuyumbishwa na wana CCM wachache wasiokubali mabadiliko anaonekana kufumbia macho utekelezaji wa kile mwanafalsafa Mwalimu nyerere alichokisema—kwamba Watanzania wanataka mabadiliko.

Mfano Rais Kikwete alipata fursa ya kusimamia mabadiliko kwa kuandika Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi.  Lakini kikundi kidogo cha wahafidhina ndani ya CCM kilimtisha akajikuta anaweka pembeni ujasiri wake aliokuwa nao wa kusimamia mabadiliko hayo muhimu kwa maendeleo ya taifa hili.

Kama uamini jiulize ni kwa   nini  Kikwete aliachia Bunge la Katiba lililojaa asilimia 80  ya wanachama likazika Rasimu ya Katiba ya wananchi pale Dodoma mwaka jana 2014  — Rasimu ambayo ingeleta Katiba yakuweka  misingi ya kuleta madadiliko Tanzania—mabadiliko ya kuhakikisha kikundi kidogo cha watawala hakijitajirishi kwa ufisadi na kujigawia mali  za umma huku mamilioni ya wananchi wakibaki maskini na mafukara wa kutupa?

Baada ya Kikwete kupoteza fursa  ya kuleta mabadiliko  kwa kuandika Katiba Mpya,  umma uliofukarishwa  umeendelea kupata uelewa kuwa CCM na serikali  yake ndicho chanzo cha umaskini wao.

Hivyo ili kuendelea  kubaki madarakani  serikali ya CCM  imekuwa  ikijihusisha na ufisadi ili ipate fedha za kuwarubuni walala hoi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Mfano mwaka 1995 Rais Benjamini Mkapa alijikuta serikali yake ikifanya ufisadi  katika  akaunti EPA (bilioni 122) zilizotumiwa na CCM kumuweka  Kikwete madarakani.

Ukitafakari utaona kwamba katika ufisadi Tegeta escow, serikali ya CCM imekapua billion 306 mara tatu ya ufisadi wa EPA mwaka 1995 ilipokwapua bilioni 122 ili kipate fedha nyingi zaidi la kuwalaghai wapiga kura mafukara ambao wameendelea kupata uelewa kuwa CCM inaiba fedha za umma kununua wapiga kura wakati wa kampeni za uchaguzi.

Hivyo serikali ya CCM inayoongozwa na Kikwete ambayo imeshuhudia nguvu ya wananchi kudai mabadiliko ikiwa kubwa kuliko wakati mwingine wowote, inajaribu kila mbinu chafu na safi ili CCM ibaki madarakani baada ya uchaguzi mwaka huu.

Ndiyo sababu  serikali ya CCM  kupitia msemaji wa chama hicho Nape Nnauye imeanza kuwaambia Watanzania kuwa  CCM lazima ishinde uchaguzi wa mwaka huu hata kama ni kwa kutumia goli la mkono (wizi au lolote lile chafu).

Zaidi  Rais   Kikwete  amefikishwa mahali  pabaya  kulazimika  kubuni  mchezo  mchafu kujaribu kuwadanganya Watanzania  kuwa eti  CCM na serikali yake ni safi, haijihusishi na ufisadi unaofukarisha wananchi isipokuwa wanachama wachache wa CCM ndio mafisadi.

Ili  kujaribu kutafuta kujenga  uhalali wa CCM kubaki madarakani baada ya uchaguzi wa  mwaka huu 2015, Kikwete amejikuta akilazimika  kumtoa  kafara Lowassa  kwa kumpakazia  ufisadi wa  Richmond.

Wananchi wanauliza kama Lowassa alikuwa ndiye mhusika  wa Richmond  ni kwa nini   Spika wa Bunge  Anna Makinda (mmoja wa watawala  wa CCM),  hakuagiza  tume ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa CCM Harrison Mwakyembe kumhoji Waziri Mkuu  Edward Lowassa?

Pili wananchi wanahoji kama CCM haijamtoa Lowassa kafara  kwa kumbebesha ufisadi wa chama hicho  ili kupumbaza hasira ya  wananchi dhidi ya ufisadi wa CCM kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu 2015  ni kwa nini  Rais Kikwete alikubali Waziri wake Mkuu  Edward Lowassa  ajiuzulu kwa ufisadi wa Richmond 2008 wakati ufisadi wa kutisha  ulifanywa na serikali ya CCM kwenye akaunti ya Tegeta escrow 2014  Kikwete aliwatetea mawaziri  waliogawiwa fedha hizo na Ikulu ilikuwa ndiyo mtuhumiwa namba moja?

Mimi si mwanasiasa wa chama chochote cha siasa hapa nchini ninachoangalia ni chanzo cha umaskini wa wananchi wengi Tanzania.

Ndiyo sababu Watanzania wengi nikiwepo mimi mwenyewe kwa sababu  tulipewa habari nusu nusu zilizotolewa kimkakati na serikali ya CCM kuhusu kashfa ya Richmond  kumpakazia Lowassa ufisadi, tulipubwazwa tukaisaidia CCM  kumchafua Lowassa kuwa ni fisadi wa Richmond.

Lakini baadhi ya wananchi walianza  kujua kuna ukweli uliofishwa kuhusu Richmond pale TV moja ilipokuwa imemwalika Lowassa aotoe yake ya moyoni live siku chache baada ya  kujiuzulu, lakini kipindi hicho cha TV kikafutwa ghafla.

Hata hivyo ukweli huo umekuja kujulikana mwezi Julai mwaka huu Lowassa alipotoa hadharani baada ya kuachana na CCM na kujiunga na CHADEMA.

Sasa wananchi    wamefahamu kuwa  CCM  chini ya serikali ya Rais Kikwete iliamua kumtoa Lowassa kafara kwa kumpakazia ufisadi wa   Richmond  ili  kuiokoa CCM isiadhibiwe vikali na wananchi kwenye sanduku huru la kura  –kwa ufisadi alinawasababishia umaskini na ufukara.

Ndiyo sababu  hivi sasa  CCM na baadhi ya wanahabar wanapakazia  CHADEMA  na  UKAWA  kuwa  eti ni mafisadi   baada ya kumpokea Lowassa (kafara wa CCM)  na  kumpitisha kuwa mgombea wa  Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Isitosha hivi sasa kikundi  cha watawala wachache wa serikali ya CCM wanahaha na wanamzonga Kikwete azuie mabadiliko kwa mkono kwa  kufanya kila uchafu  kupumbaza Watanzania kwa kutumia kete ya eti   Lowassa ni  fisadi wa  Richmond  hivyo hana sifa ya kugombea Urais wa Tanzania,  bali Magufuli ndiye mtu safi.

Wananchi wenye akili zao wanajiuliza hivi mwenye kashfa za kifisadi kati ya Lowassa na Magufuli ni nani?  Ni Lowassa aliyepakaziwa Richmond au ni Magufuli aliyeongoza watawala kujiuzia kwa bei chee nyuma za umma zilizogarimu wanannchi mabilioni ya fedha?

Wananchi pia wanajiuliza kama Lowassa ni fisadi wa Richmond ni kwa nini serikali ya CCM haijamshitaki mahakamani miaka minane tangu ufisadi huo ulipotokea?

Hivyo  pengine  baada ya Lowassa kutafakari nafsi yake na kuona kuwa CCM imemtoa kafara asigombee Urais  ili kuzuia mabadiliko, ameamua kufanya  maamuzi magumu  ya kuhama CCM  –kushiriki kuongoza masikini  na mafukara  wanaotafuta mabadiliko.

Lowassa ameamua kutekeleza alichokitabiri Mwalimu Nyerere kwamba CCM isipokubali kuongoza wananchi wapate mabadiliko wanayoyataka—wananchi watayatafuta mabadiliko hayo  nje  ya CCM.

Ni dhahiri CCM ilipoteza fursa adimu ya kuongoza wananchi kwenye kuleta mabadiliko kwa kuandika Katiba  Mpya– kuweka  misingi ya kukomesha mfumo wa utawala  unaowezesha watawala kuwa matajiri wa kupindukia  huku mamilioni ya wananchi wakiwa mafukara na nchi ikinuka aibu ya umaskini  wa kijitakia  ikiwa rasilimali nyingi za asili.

Wanaomchochea Rais Kikwete asikubali mabadiliko yachukue mkondo wake, wameunda timu ya kampeni yanye wajumbe wengi waliohusika kumpakazia Lowassa ufisadi wa Richmond ili eti kwenye kampeni waendelee kumpaka ufisadi  Lowassa, CHADEMA na UKAWA wakidhani Watanzania hawana akili ya kutafakari.

Lengo lao ni moja. Wanajua kabisa kuwa kwa kutumia sanduku huru la CCM  haiwezi kuchaguliwa. Wanataka kutumia kisingizio   kuwa  CHADEMA  na UKAWA imechafuka eti kwa kumsimamisha Lowassa Urais  ambaye CCM imemtoa karafa – kwa kumpakazia ufisadi wa Richmond.
Lakini baada ya kupata salamu za wananchi kupitia mafuriko yao kwenye kumtambulisha Lowassa kwamba wao wanaelewa fisadi kamili ni CCM, sasa CCM imeshtuka imeanza kutumia polisi kuwaadhibu wananchi. Pengine baadaye itatumia jeshi kabisa.

Zaidi imeamua kujaribu kampeni za   ardhini -nyumba kwa nyumba, bila shaka kutumia mabilioni ya fedha serikali ya CCM ilizokwapua Tegeta escrow kununua shahada na kura za mafukara.

Kwenye kampeni za   nyumba kwa nyumba mtu kwa mtu ndiko ufisadi mbaya wa kisiasa unakofanyika—kununua, kutisha na kuumiza    wananchi mafukara.
Swali ni je Watanzania wangapi wapiga kura watakubali CCM inapopita majumbani mwao kuuza shahada zao  kwa sukari, kanga au fedha hata kama CCM itaamua kumpa kila mpiga kura shilingi milioni moja?

Ni mpiga kura gani atakayekubali KUDANGANYIKA  kwa  kununuliwa na  CCM  kwa vijizawadi vya fedha nguo KUSALITI   mamilioni ya watanzania  wanaoendelea kuteseka  kwa ufukara kila baada ya uchaguzi kwisha na CCM kubaki madarakani?

Wananchi  pia wanauliza je mabilioni ya escrow yatawanunua wajumbe wa NEC ili  wavuruge daftari la wapiga kura, au wachakachue kama uchaguzi wa 2010  au wataharibu daftari la wapiga kura, mashine   na vifaa vya kupigia kura, au kuchelewesha kwa makusudi kufungua vituo vya wapiga kura  ili  kuvuruga uchaguzi CCM  ishinde kwa goli la mkono?

Kadhalika wananchi wanauliza wanaomshinikiza Kikwete asikubali mabadiliko wakiona hilo haliwezekani je watamuua Lowassa waliomtoa kafara au  viongozi wa CHADEMA na UKAWA waliompokea Lowassa na kumwezesha kufikia azma yake ya kujitolea kuwatumikia watanzania  ili kuvuruga uchaguziwa mwaka huu?

Wananchi wanauliza maswali hayo  baada ya kubaini kwamba huenda  wasiomtakia mema Kikwete astaafu kwa amani  wamejaribu kuwalaghai baadhi ya viongozi wakuu wa UKAWA ili kujaribu kuvuruga UKAWA – lakini UKAWA kwa vile ni sauti ya mafukara-sauti ya umma  imeendelea kuwa moto mkali wa nyika  dhidi ya CCM.

Hivyo binafsi namshauri Rais Kikwete akubali kuwa baba wa pili wa Taifa hili baada ya Nyerere kuondoka. Akubali kusimamia wananchi watumie sanduku huru la kura kwenye uchaguzi wa mwaka huu 2015 kupata mabadiliko ya uongozi wanayoyataka.

Wananchi wana imani na UKAWA   kwamba wakiingia madarakani Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi itaandikwa.

Huo utakuwa ni mwanzo wa mabadiliko wanayoyataka wananchi—kuhakikisha watawala hawajitajirishi kupindukia kufisadi fedha za wananchi huku wananchi wengi wakibaki mafukara.  CHADEMA  na UKAWA  wasipotimiza hili na kuonyesha  kwa vitendo maendeleo watakayokuwa wameyaleta kwa miaka mitano, ni lazima wananchi watatumia sanduku la kura kuwapunzisha.

Ninaamini ni wenye kutetea maslahi binafsi tu ndiye atakayemlaumu Rais Kikwete kwamba eti CCM isipochaguliwa Oktoba 25, Kikwete atakuwa ni chanzo  cha wananchi kuamua kuipunzisha CCM  kwa miaka mitano.

Nitakuwa wa kwanza kuwapinga watu hao na kumtetea Kikwete hata kama ni kwa kuamua  kuingia kwenye siasa  kwa kujiunga na CCM .

Hakika Rais Kikwete  ukisimamia  wananchi  wazungumze kuhusu hatma ya uongozi wan chi yao kwa kutumia sanduku huru la kura  bila CCM kuingiza  mkono mchafu, wewe mwenyewe ukistaafu utaishi kwa amani na furaha huku baadhi yetu tukikuona kama baba wa Pili Taifa taifa hili, baada ya Mwalimu Nyerere.

Mwisho ninaruhusu yeyote anayetaka kuchapisha au kutangaza redioni natelevisheni niyoyoyaandika hapa TV au kuchapisha na kuwasambazia Watanzania wote popote walipo ujumbe huu afanye hivyo. Wanawaza kuwasambazia watu mitaani, kwenyemikutano ya kampeni, mashuleni vyuoni popote pale—lengo likiwa moja—sote Watanzania tuujue ukweli kuhusu ufisadi na mchango wake katika kuwafanya Watanzania waishi katika umaskini.   Lakini muhimu kila Mtanzania ajue hakuna mshindi wa kujisifu—mshindi ni  nchi yetu Tanzania na  Watanzania  wote.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

– Ananilea Nkya

E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com

 

Acha maoni yako kuhusu kwa kutumia fomu hapa chini

2 Maoni

  1. ikiwa lowasa alitolewa na kamati ya maadili na wengine akiwemo mizengo pinda inaonekana dhahiri mizengo pinda hana nidhamu ilkuwaje serikali ya ccm ilimteua kuwa waziri mkuu

Weka majibu hapa

Tafadhali weka maoni
Tafadhali weka majina yako hapa