LOWASSA KAMA SAULI

0
826

Fred Mpendazoe kwenye gazeti la Raia mwema toleo la 417
 la tarehe 5 Aug 2015 kaandika hivi:

NIMEONA ni vema niandike makala hii baada ya kupigiwa simu nyingi sana na wasomaji wa Raia Mwema baada ya Edward Lowassa kuhamia Chadema. Wengi wameomba maoni yangu na wengine uchambuzi.
Katika makala hii mimi nitaeleza maoni yangu tu. Nilikuwa nimeanza kuandika makala juu ya tabia ya unafiki ya wana CCM ambao kila mara hunukuu maandiko kadhaa ya Hayati Mwalimu Nyerere kwenye hotuba zao kwenye majukwaa na mikutano ya kisiasa lakini ukiwaambia wahame CCM wanakataa kata kata. Mimi nilikuwa najiuliza hawa wanamuenzi vipi.
Wakati wa huduma ya Nabii Issa ilipokuwa inafikia ukingoni, siku moja Nabii Issa alikamatwa akawekwa gerezani kutokana na mpango uliokuwa umeandaliwa kwa muda mrefu na mafarisayo na masadukayo ambao wengi wao walikuwa ni viongozi wa dini.
Kwa kifupi, falsafa za Nabii Issa zilikuwa zinapingana na mwenendo wa mafarisayo na masadukayo wakati ule. Humo gerezani au rumande Nabii Issa alikutana na Barnaba ambaye alikuwa amefungwa kwa ajili ya tuhuma za wizi au ufisadi.
Kama ilivyokuwa desturi wakati ule, Pilato alitakiwa atoe hukumu kwa Nabii Issa. Pilato aliangalia tuhuma za Nabii Issa na alibaini tuhuma hazikuwa na ushahidi, hivyo akataka amwache huru. Pilato aliwauliza wale watu waliokuwa wamekusanyika kwamba amwachie nani kati ya Barnaba na Nabii Issa. Umati uliokuwepo pale ukiongozwa na mafarisayo na masadukayo walipiga kelele kwa nguvu, wakisema amwachie Barnaba! Hivyo, Barnaba akatolewa gerezani kwa shinikizo la umati wa watu.
Sababu iliyosababisha mafarisayo na masadukayo na Wayahudi wengine wamtake Pilato amwachie Barnaba ambaye walikuwa wanajua ni mwizi au fisadi ni tabia yao ya unafiki. Tunaambiwa mafarisayo na masadukayo walikuwa na elimu ya kutosha, elimu ya dini na elimu ya kawaida.
Pia walijihesabia haki ya kupitiliza. Tatizo kubwa la mafarisayo na masadukayo ilikuwa unafiki, yaani kuishi maisha ambayo yalikuwa tofauti na walivyokuwa wakihubiri na tofauti na elimu waliyokuwa nayo. Walikuwa ni wanafiki kupindukia.
Mafarisayo walikuwa wakipita barabani wakisali sala ndefu ili waonekane. Kwenye masinagogi walikaa viti vya mbele. Walipotoa sadaka makanisani, walitoa fedha nyingi kwa kuonekana ili wasifiwe.
Walipokuwa wakisali, walisali kwa sauti kubwa ili maneno yao yasikike, walipangilia sala zao vizuri kwa ufasaha ili wasifiwe. Lakini, maisha halisi ya mafarisayo na masadukayo yalikuwa ni machafu, yaliyojaa ufisadi. Mahubiri ya Nabii Issa yaliwakasirisha sana mafarisayo na masudukayo kwani aliweka wazi unafiki wao.
Walikataa mahubiri yake. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu kuu ya kumtaka Barnaba atolewe gerezani na kumkataa nabii Issa. Lakini kwa kumkataa nabii Issa, Israel inasumbuka mpaka leo.
Ndani ya CCM, kuna kundi la wana CCM wazee ambao wanatambua kwamba CCM imefika mwisho, imechoka, imekosa mwelekeo na imepoteza sifa na heshima ya kuendelea kuongoza nchi. Wana CCM hawa wamekuwepo ndani ya CCM toka wakati wa hayati Mwalimu Nyerere.
Wanatambua tofauti ya CCM ya leo na CCM ya Nyerere. Wazee hawa katika majukwaa mbalimbali wanaikosoa sana CCM na serikali yake. Je ni nini tofauti ya wana CCM hawa na mafarisayo wa Uyahudi waliomtoa Barnaba gerezani?
Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaambia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, na baadhi ya wazee ninaowazungumzia walikuwepo nanukuu “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata, wasipoyaona ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM”. Baada ya kuwaambia maneno haya, wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya CCM wakiwemo wazee wetu walishangilia sana.
Sijui kwa nini walishangilia, kwani tafsiri ya maneno haya ni kwamba kama CCM itashindwa kuleta mabadiliko basi Watanzania watayatafuta mabadiliko hayo kwenye vyama vya upinzani. Aidha, Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, na wazee hawa walikuwepo “Bila CCM madhubuti nchi itayumba”.
Ni bayana kwamba CCM ya leo siyo imara tena. Na ni dhahiri nchi yetu imeyumba kutokana na uongozi legelege wa CCM. Kwani chama legelege huzaa serikali legelege.
Ninaamini pasipo shaka yoyote Nyerere angekuwepo leo asingekuwa mwana CCM. Angekuwa upinzani au raia asiye mwanachama wa chama cha siasa. Lakini siyo CCM ya leo. Lakini, wazee hawa kila mara huwa wanasema wanamuenzi Mwalimu Nyerere. Lakini tujiulize, kwa lipi?
Wanamuenzi kwa kuendelea kuwa wanachama wa CCM iliyochoka na kuacha misingi yake? Wanamuenzi kwa kuendelea kuwa wanachama wa CCM na serikali yake inayonyanyasa wakulima na wafanyakazi?.
Ikiwa CCM si madhubuti tena wanategemea nini tena wakati ni bayana mabadiliko hayataletwa na CCM? Au nao wazee hawa ni mafarisayo wa Uyahudi? Au wanayoyahubiri kwenye majukwaa si yale wanayoyaishi? Ipo siku waliyoyaficha kwa siri sana yatakuwa hadharani. Lakini ninawasihi wazee wetu, njia ya heshima ya kumuenzi Mwalimu Nyerere siyo kubaki CCM. Nawasihi watoke CCM.
Ninafahamu kwamba tuna mitazamo tofauti ya mawazo. Dhamira zetu pia hazilingani na hatuna sare za mawazo kwa wakati wote. Nitumie mfano kufafanua suala la wale ambao wamebaki ndani ya CCM ambayo imeyumba hususani wazee waliofanya kazi na Nyerere.
Tunamfahamu Musa kwenye Maandiko Matakatifu. Inaelezwa kuwa alipokuwa mtu mzima alikataa kuitwa mwana wa binti Farao, akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na wana wa Israeli kuliko kujifurahisha kwa kitambo kwenye Ikulu ya Farao, ambaye alikuwa anawanyanyasa Waisraeli na ndugu zake. Musa aliondoka kwa Farao, ikulu iliyojaa neema.
Ndani ya CCM kumechafuka. CCM na seriklai yake inawanyanyasa Watanzania. Ni jambo la kushangaza kuona wazee waliofanya kazi na Hayati Mwalimu Nyerere wanaona fahari gani kuendelea kukaa kwenye chama ambacho kimeacha misingi yake.
Wengine wameendelea kubaki humo na mnawasikia wakipiga kelele kwamba wanaonewa. Ni rahisi kwa mtu yeyote kufikiria kwamba maslahi yao binafsi ni muhimu kuliko kuwatetea wananchi. Msanii maarufu wa Ufaransa, Cocteau, aliwahi kusema: “Ni hulka ya jamii nyingi kunyamazisha sauti huru za wapenda haki. Kwanza, zitajaribu kukushambulia kwa kukupiga. Hilo likishindikana kukunyamazisha, zitajaribu kukuua kwa kukuwekea sumu. Hilo, nalo, likishindikana, zitamalizia kwa kukumwagia sifa, heshima, tuzo na vyeo”.
Inawezekana tuzo na vyeo ndiyo sababu ya kuendelea kubaki CCM. Wako wapi leo wapambanaji 11 wa ufisadi mliowasikia mwaka 2008 na 2009? Wengine ni mawaziri, wengine ni manaibu waziri, wengine ni viongozi kwenye CCM.
Ni nini tofauti yao na mafarisayo wa Uyahudi waliomtoa Barnaba gerezani?. Lakini pia wapo waliondelea na mapambano.
Lowassa alikuwa mwana CCM aliyekulia na kutumia muda mwingi wa maisha yake akiwa CCM. Lowassa aliipenda CCM na aliipigania. Namfafananisha Lowasaa na Saul Mwebrania, msomi wa kupindukia aliyekuwa anaupenda mfumo wa kiutawala wa wakati huo na akaupigania kama Lowassa alivyoipigania CCM na serikali yake.
Kwa kifupi, Sauli alikuwa ni mmoja wa viongozi ambao walikuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera na mipango ya serikali ikiwemo kuhakikisha wafuasi wa Yesu au Wakristo wanadhibitiwa na hata kuangamizwa.
Siku moja Sauli akiwa katika kutekeleza maagizo ya kuwatesa Wakristo alikutana na muujiza ambao matokeo yake ulisababisha Sauli abadili msimamo na hatimaye akawa moja ya wahubiri wakuu wa injili ambayo alikuwa akiipinga. Kwa neema ya Mungu, Sauli aliweza kubadilika.
Wakati wa kumkaribisha Lowassa Chadema, Mwenyekiti wa Chadema alisema ilikuwa si kazi rahisi kumshawishi Lowassa kujiunga na Chadema. Kwa maoni yangu nasema Lowassa kuhamia Chadema ni kwa neema ya Mungu na binadamu yeyote asije kujisifu.
Nawakumbusha tena, ndani ya CCM kuna kundi la wana CCM wazee ambao wanatambua kwamba CCM imefika mwisho, imechoka, imekosa mwelekeo imepoteza sifa na heshima ya kuendelea kuongoza nchi.
Wana CCM hawa wamekuwepo ndani ya CCM tangu wakati wa hayati Mwalimu Nyerere. Wanatambua tofauti ya CCM ya leo na CCM ya Nyerere. Wazee hawa katika majukwaa mbalimbali wanaikosoa sana CCM na serikali yake, lakini ukiwaambia ondokeni huko hawaelewi wanasema watafia humo.
Ukiwauliza kwa nini wanasema wanamuenzi Mwalimu. Ukiwauliza kwa lipi? Hawana la kujibu. Naamini ipo siku Neema aliyoipata Lowassa nao wataipata na hatimaye wataihama CCM na hapo watakuwa wanamuenzi Mwalimu kwa uhalisia.
Sauli alipoanza kuihubiri injili aliyokuwa akiipinga awali watu wengi walishangaa sana na hata baadhi ya Wakristo walimnyanyapaa. Ndivyo ilivyo kwa Lowassa. Wapo wana Chadema hawakubaliani na Lowassa kuhamia Chadema. Wanalalamika. Lakini tukumbuke kwamba kule mbinguni huwa ni sherehe mwenye dhambi mmoja akibadilika.
Malaika mbinguni hawalalamiki kwa mwenye dhambi kuhama kutoka ufalme wa giza kwenda ufalme wa Mungu, hushangilia. Lowassa amebadilika, wana Chadema tumpokee.
Lowassa kuhama CCM ni muujiza, ni kwa neema sawa na Sauli wa Tarso kuiamini injili aliyoipinga. Hata kama alikuwa mchafu kiasi gani, yeye ameikana CCM na mambo yake yote, tumpokee. Kumbukeni, Sauli aliyewatesa Wakristo ndiye ambaye ameandika nyaraka nyingi na kuwafanya Wayahudi wengi waiamini Injili.
Sauli ambaye alikuja kuitwa Paulo alifanya kazi kubwa zaidi kuliko mitume walioanza na Yesu. Biblia inasema wa kwanza atakuwa wa mwisho, na Katiba ya Chadema inasema mwanachama wa Chadema aliyeingia miaka 20 iliyopita na aliyejiunga mwezi mmoja wote wana haki sawa, hivyo kama Lowassa anazo sifa za kuipatia Chadema ushindi agombee urais na wanachadema tumuunge mkono.
Namfahamu Lowassa kwa muda mrefu, nimefanya kazi naye kwa miaka minane pale Wizara ya Maji. Ana sifa moja kuu, ni jasiri. Nilikuwa mbunge wakati alipopata kashfa ya Richmond.
Niliiamini Ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Felix Mwakyembe Mwakyembe kama Watanzania wengine walivyoamini na kumhukumu. Lowassa ameeleza hahusiki, aliwajibika kisiasa.
Tumwamini. Marafiki za Lowassa watakaohamia Chadema wafanye ungamo lao na wapimwe imani yao.
Lowassa ana kazi moja kubwa inayohitaji neema tena. Anatakiwa kuwasamehe kwa dhati wote waliomhukumu na mmoja wao ni mimi kwa makala zangu kali. Lakini pia Lowassa amshukuru Mungu kwa Kamati Kuu ya CCM kuliondoa jina lake, kwani hapo ndipo mpango wa Mungu ulikuwa unatimia kwa yeye kuwa mgombea urais jambo ambalo lisingewezekana ndani ya CCM.
Kumbukeni Josefu aliuzwa utumwani Misri na kaka zake. Josefu aliumia sana. Lakini ilibidi awasamehe kaka zake waliofanya mpango wa kumuuza. Lakini Josefu ilibidi auzwe utumwani ili aje kuwa Waziri Mkuu wa Misri.
Lowassa amepitia misukosuko na mambo mengi magumu sana, ninaamini ni kwa ajli ya kuandaliwa kwa kuwatumikia Watanzania. Jina la Lowassa liliondolewa na watu waliokuwa ni wa karibu na yeye, marafiki zake, viongozi wenzake. Dhahabu ili iwe na thamani kubwa hupitishwa kwenye tanuru la moto mkali.
Naiona ndoto aliyonayo Lowassa ya kuwa rais inatimia. Akipitishwa na Ukawa tumuunge mkono.

Leave your comment about LOWASSA KAMA SAULI using the comment form below

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here