Magazeti ya Mtanzania na Mwananchi Yafungiwa

5
3466
Gazeti la Mwananchi Lafungiwa.

TAMKO LA SERIKALI

Serikali imeyafungia  kutochapishwa Magazeti ya MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba,2013  kutokana na mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala  za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha amani na mshikamano ulipo nchini.

Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kutochapishwa kwa siku kumi na nne(14) kuanzia 27 Septemba,2013.Adhabu hii imetangazwa kwa Tangazo la Serikali(Government Notice )Namba 333 la tarehe 27 septemba,2013.

Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani,mfano tarehe 17 Julai,2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari isemayo “MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013”  kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri  haukupaswa kuchapishwa Magazetini.

Aidha, katika toleo la Jumamosi,tarehe 17 Agosti,2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho “WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI”  habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa  mkali mwenye hasira.Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka Mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya kiislam.Jambo ambalo halikuwa la  ukweli.

Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti.Serikali na jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi lake haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.

Hivyo basi,kwa gazeti hili kuchapisha habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya kiislam  mbwa ni najisi hapaswi kuingia  katika maeneo ya ibada.
Magazeti ya Mtanzania na Mwananchi zafungiwa.Gazeti la MTANZANIA limefungiwa kutochapishwa kwa siku tisini(90) kuanzia tarehe 27 Septemba,2013 kwa kuchapisha habari zenye uchochezi.Gazeti hili limeonywa mara nyingi  lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa  kichochezi na lizingatie maadili na Sheria na Kanuni za  fani ya Habari.
Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonyesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika toleo na 7262 la 20 Machi,2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA DAMU”, tarehe 12 Juni,2013, toleo Namba 7344 lilichapisha makala isemayo “MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”.
Aidha, siku ya Jumatano,tarehe 18 Septemba,2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha Kichwa cha habari kisemacho “SERIKALI YANUKA DAMU” taarifa hiyo ilikolezwa na picha zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta  kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika .Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika  na wahanga waliomizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na  waliyovamiwa na kujeruhiwa vibaya.
Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi.
Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama  wavione kuwa haviwasaidii.
Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu serikali imelifungia gazeti la Mtanzania  kutochapishwa kwa muda wa siku tisini(90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332(Government Notice No.332) la tarehe 27 septemba,2013,.
Serikali inawataka wamiliki,wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini,kuzingatia weledi,miiko na madili yataaluma uandishi wa habari.
Serikali inawataka wamiliki na hasa wahariri kuhakisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia taaluma,kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu.
Serikali inavionya vyombo vya habari vinavyoutumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo ya kuvifungia .Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani  nchini.
Imetolewa na

MKURUGENZI IDARA YA HABARI
WIZARA YA HABARI,VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
28 SEPTEMBA,2013

Kutoka Mitandaoni

Mtanzania
http://www.mtanzania.co.tz/
‘Vinasaba vitaonyesha kama Watanzania walikufa Kenya’. Jumamosi, Septemba 28, 2013 06:05 Na Sarah Mossi na Esther Mbussi. BALOZI wa Tanzania nchini 

MICHUZI BLOG
http://issamichuzi.blogspot.com/
45 minutes ago NEWS ALERT:Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania yafungiwa 7262 la 20 Machi,2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS 

wavuti.com – Blog
http://www.wavuti.com/
53 minutes ago Serikali imeyafungia kutochapishwa Magazeti ya MWANANCHI na MTANZANIA kuanzia 27 Septemba, 2013 kutokana na mwenendo wa 

Mwananchi: mwanzo – Gazeti la habari za kiswahili la kila siku …
http://www.mwananchi.co.tz/
Skip to the navigationchannel.links.navigation.skip.label. Skip to the content. MCL Blog|Daily Nation|NTV|Business Daily|The East African|Daily 

 

Leave your comment about Magazeti ya Mtanzania na Mwananchi Yafungiwa using the comment form below

5 COMMENTS

 1. TAARIFA YA NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA,

  UTAMADUNI NA MICHEZO, MH. AMOS MAKALLA

  KWA VYOMBO VYA HABARI

  Napenda kuufahamisha umma kwamba mimi ndiye NILIYERUHUSU Gazeti la Mwananchi kuendelea na utoaji wa taarifa/habari kwenye tovuti yake, pia Gazeti la Rai kutoka kila siku.

  Ninalazimika kutoa ufafanuzi kwa njia ya maandishi kutokana na kupigiwa simu nyingi na waandishi wa habari kuhusiana na tamko jipya la Mkurugenzi wa Habari – Maelezo, Ndg Assah Mwambene kuhoji uhalali wa Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku, badala ya mara moja kwa wiki (Alhamisi).

  Tarehe 4/10/2013 nilifanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL) na New Habari Corporation (2006) Ltd kwa upande mmoja na msajili wa magazeti kwa upande mwingine.

  Katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania maombi matatu yaliwasilishwa;

  1. Ombi la kumuomba waziri apitie upya adhabu iliyotolewa kwa mageazeti hayo. Katika hili Majibu yangu niliwaambia kwamba mwenye mamlaka juu ya suala hilo ni waziri mwenye dhamana na masuala ya habari pekee.

  2. Ombi la Gazeti la Mwananchi kuwa online na Gazeti la Rai kutoka kila siku badala ya kutoka siku ya Alhamis.

  2.1 New Habari walieleza kuwa siku zilizopita waliwahi kuomba kwa maandishi (barua) kwamba gazeti la Rai litoke kila siku. Maelezo ya Naibu Msajili wa Magazeti katika kikao hicho yalikuwa kwamba, kulikuwa na tatizo la kiufundi katika kurejea maombi hayo na akakiri kuwa hakuna kinachozuia gazeti la Rai kutoka kila siku. Kutokana na maelezo hayo mimi niliridhia gazeti hilo sasa liruhusiwe kutoka kila siku.

  2.2 Kuhusu gazeti la Mwananchi kuwa online, Naibu Msajili alisema hakuna sheria yeyote inayoweza kuzuia gazeti hilo kuwa online ila aliwataka lisionekane gazeti zima kama lilivyo pia wabadili nembo (Master Head) kwamba waweke nembo ya MCL na siyo ya gazeti husika ambalo limefungiwa. Pia baada ya maelezo hayo niliridhia gazeti hilo liwe mtandaoni kwa kuzingatia angalizo lililotolewa na Naibu Msajili wa Magazeti.

  3. Hoja ya tatu ilikuwa ni ile ya Serikali kupitia Idara ya Habari – Maelezo kuwa na uhusiano mzuri na vyombo vya habari, ili kuepuka misuguano isiyo ya lazima.

  3.1 Pendekezo hili nililipokea na niliwasilisha kwa Mhe Waziri wa Habari kwa hatua zaidi, likiwamo suala la kupitia upya adhabu na ushauri wa kujenga uhisiano na vyombo vya habari.

  3.2 Masuala ya Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai kutoka kila siku, NILILITOLEA UAMUZI siku hiyo hiyo, na uamuzi ni kwamba niliwaruhusu baada ya kuridhika kwamba hakukuwa na ukiukwaji wa sheria yoyote uliofanywa na waombaji.

  Nimeamua kuweka sawa jambo hili kutokana na taarifa ya Mkurugenzi wa Maelezo ambayo ninaamini kwamba kutolewa na kusambazwa kwake ni kukosekana kwa mawasiliano kati yake kwa uipande mmoja na Mhe. Waziri, Naibu waziri na Naibu Msajili wa Magazeti kwa upande mwingine.

  Hivyo aliyeruhusu Gazeti la Mwananchi kuwa online na Rai ni mimi na ndiyo maana kuanzia tarehe 5/10/2013 Gazeti la Rai lilianza kuchapwa kila siku na kusambazwa, na Gazeti la Mwananchi likaanza kuwa mtandaoni kwa kuzingatia maelekezo ya Naibu Msajili wa Magazeti.

  Imetolewa na:

  Amos G. Makalla

  Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo

  11 Oktoba 2013

 2. TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

  Idara ya Habari – MAELEZO, inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kwamba Mheshiwa Dkt. Fenella Mukangara, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo amepokea maombi kutoka kwa wamiliki wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania wakiomba kupunguziwa adhabu au kusamehewa adhabu wanazozitumikia kuanzia 27 Septemba, 2013.

  Wakati Mheshiwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo anatafakari maombi hayo, amesikitishwa kuona kwamba magazeti haya mawili yamekiuka masharti ya adhabu walizopewa.

  Wamiliki wa Gazeti la Mtanzania baada ya kufungiwa wameamua kuligeuza gazeti la kila wiki la RAI kuwa la kila siku bila ya kibali cha Msajili wa Magazeti. Kwa mujibu wa ratiba ,gazeti la RAI linapaswa kutoka kila siku ya Alhamisi.

  Wamiliki wa gazeti la Mwananchi nao wameendelea kuchapisha gazeti hilo katika mtandao kinyume na agizo la kufungiwa.

  Serikali inawataka wamiliki wa vyombo habari nchini kuwa na utamaduni wa kutii sheria za vyombo vya habari zinazotumika wakati huu. Hivyo serikali kwa mara nyingine tena inawataka wamiliki wa Gazeti la MTANZANIA, kuzingatia ratiba yao ya kutoa gazeti lao kila siku ya ALHAMISI.

  Aidha, serikali inawataka wamiliki wa Gazeti la Mwananchi kuacha mara moja kuchapisha gazeti lao katika mtandao kama amri ya kufungiwa ilivyoanisha.

  Imetolewa na,
  Idara ya Habari – MAELEZO

 3. TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
  kama mnavyofahamu, Serikali imeyafungia magazeti ya Mtanzania na Mwananchi kwa kuzingatia Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 na kanuni zake za mwaka 1977. Gazeti la Mwananchi limefungiwa kwa muda wiki mbili kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013 na Gazeti la Mtanzania limefungiwa kwa muda wa miezi mitatu au siku 90 kuanzia tarehe 27 Septemba,2013.
  Aidha tunataka umma ufahamu kuwa Serikali haikukurupuka kufungia magazeti hayo. Uamuzi huo ulifanyika baada ya kufuata taratibu zote za msingi ikiwemo kuwasikiliza wahusika.
  Hata hivyo, tumeona gazeti la Mwananchi baada ya kufungiwa limeendelea kuchapishwa kwenye mtandao wa Internet kinyume cha amri iliyotolewa .Kufanya hivyo ni kosa na Serikali tumewaandikia kuacha mara moja la sivyo, Serikali italazimika kuchukua hatua kali zaidi.
  Aidha kampuni ya New Habari 2006 baada ya kufungiwa moja ya magazeti yake, imeanza kuchapisha gazeti la ‘Rai’ kila siku tangu tarehe 29 Septemba mwaka 2013 bila ya kibali cha Msajili wa Magazeti. Hilo nalo ni kosa, Serikali inawataka kuacha mara moja kuchapisha gazeti hilo kila siku na warudie ratiba yao ya kuchapisha mara moja kwa wiki mpaka hapo maamuzi mengine yatakapofanyika.
  IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI –MAELEZO
  TAREHE 1/10/2013.

 4. KUFUNGIWA MAGAZETI – WAHAFIDHINA SASA WANAONGOZA

  Zitto Kabwe, Mb

  Kwa mshtuko na masikitiko makubwa kuanzia jana jioni tumepokea taarifa za kufungiwa kwa magazeti mawili ya kila siku hapa nchini ya Mwananchi na Mtanzania. Serikali imechukua uamuzi huo kwa kutumia sheria ya kidikteta ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo Tume ya Jaji Francis Nyalali iliiorodhesha kama sheria kandamizi. Sababu zilizotolewa kuhalalisha uamuzi huu ni sababu zisizo na maana na ambazo Serikali ingeweza kufungua mashtaka ya kawaida kabisa mahakamani kushtaki magazeti hayo iwapo haikupendezwa na habari walizochapisha.

  Moja ya sababu ya kufungiwa kwa gazeti la Mwananchi ni kuchapisha taarifa kuhusu mishahara ya Serikali. Serikali inasema habari hii ni siri. Serikali hii hii ambayo imesaini makubaliano ya kuendesha serikali kwa uwazi (Open Government Initiative) na kumwagiwa sifa na Rais Barack Obama wa Marekani inalifungia gazeti kwa kuandika habari za mishahara ya watumishi wa Serikali. Mishahara kuanzia mshahara wa Rais mpaka wa mtendaji wa Kijiji haipaswi kuwa jambo la siri. Kuonyesha kuwa jambo hili linapaswa kuwa wazi mkutano ujao wa Bunge tutatafuta kila namna kutaja mshahara wa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na baadhi ya Watendaji wa Mashirika makubwa ya Umma kama njia ya kuwaunga mkono gazeti la Mwananchi kwa habari yao hiyo. Mapato ya Mbunge yanajulikana sasa kuwa ni shilingi milioni 11.2 kwa mwezi kabla ya kuongeza posho za vikao za shilingi laki 200,000 kwa siku na posho ya kujikimu ya shilingi 130,000 kwa siku. Watanzania wana haki ya kujua wanawalipa kiasi gani watumishi wao. Tutaanza na mshahara wa Rais!

  Gazeti la Mtanzania limefungiwa pamoja na mambo mengine kwa kuandika ‘mapinduzi ni lazima’. Inashangaza Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaogopa neno mapinduzi. Marehemu Mzee Steven Salum Nandonde, aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Tandahimba alipata kusema bungeni kuwa ‘lazima nchi ipinduliwe’. Ni matumizi ya lugha tu. Mzee Nandonde yeye alikuwa analalamikia maendeleo duni ya mikoa ya kusini na kutaka Kaskazini iwe Kusini na Kusini iwe Kaskazini. Serikali inafungia gazeti kwa sababu ya kuandika Mapinduzi ni lazima ilhali kila siku Zanzibar wanasema Mapinduzi daima!

  Gazeti la Mtanzania linahaririwa na Absalom Kibanda, mwandishi wa habari ambaye bado anaponya majeraha ya mwili na kisaikolojia ya kuteswa na watu ambao mpaka leo hawajakamatwa. Badala ya Serikali kuwakamata watesaji wa Kibanda, inamnyima kazi Kibanda ili ateseke kwa njaa kwa kukaa miezi mitatu bila kazi. Pia wanatutesa Watanzania kwa njaa ya kupata habari ambayo ni haki ya msingi ya kikatiba. Hii ndio zawadi Serikali inampa Kibanda baada ya kung’olewa kucha, kunyofolewa jicho, kukatwa vidole na kuteswa kwa namna isiyoelezeka.

  Matukio ya hivi karibuni na namna Serikali inavyoyachukulia yanaonyesha dhahiri kwamba Rais Kikwete kazidiwa nguvu na kundi la wahafidhina ndani ya chama na Serikali yake. Rais ambaye alianza kwa kuhubiri uvumilivu wa hali ya juu na hata yeye mwenyewe kupata kusema uvumilivu huu wengine wanauona kama udhaifu lakini ameamua kujenga Taifa la kuvumiliana. Rais alipata kulalamika hadharani kwamba kuna wenzake wanataka aongeze ukali. Ni dhahiri kundi hili la wahafidhina sasa ndio linalomwongoza Rais Jakaya Kikwete. Kitu kimoja tu Rais azingatie, kundi hili linaongozwa na maslahi binafsi ya kubakia kwenye utawala wakati yeye anapaswa kuacha ‘legacy’. Rais Kikwete asipokuwa makini atakuwa Rais karatasi (lame duck) tu tunapoelekea mwisho wa utawala wake. Maamuzi ya hovyo na ya kidikteta ya kufungia magazeti yanamchora vibaya mbele ya wananchi na jamii ya kimataifa. Wahafidhina kuwa nguvu zaidi ya kiutawala ni makosa ambayo watanzania hawapaswi kuyakubali kamwe.

  Wananchi sasa waifanye Serikali kujutia uamuzi wake wa kufungia magazeti. Nimeamua mimi binafsi kama mbunge kesho Jumatatu tarehe 30 Septemba, 2013 kupeleka taarifa rasmi kwa Katibu wa Bunge ya kupeleka muswada Bungeni wa kuifuta kabisa Sheria kandamizi ya magazeti ya mwaka 1976. Sasa tupambane na kundi dogo la wahafidhina ndani ya Serikali na CCM wasiopenda mabadiliko na iwe fundisho kwa wahafidhina wengine wowote waliopo ndani ya Serikali au nje ya Serikali kwamba Uhuru wa habari sio jambo la kuchezea kama golori.

Leave a Reply to Mpekuzi Cancel reply

Please enter your comment!
Please enter your name here