RAIS KIKWETE JIANDAE KISAIKOLOJIA KUPOKEA TUZO YA DUNIA

0
1031
Jakaya Kikwete
Rais wangu  Jakaya Mrisho Kikwete,
Natumaini hujambo na Mungu wetu mwema anaendelea kukujalia afya njema, furaha na amani. Hongera sana kwa ujenzi wa taifa letu.
Ninakuandikia leo hii 23/09/2013 ujumbe huu wa wazi wenye  maneno  machache ambayo  yalinijia akilini mwangu usiku wa manane  na nikalazimika kuamka mapema na kuyaweka kwenye kumbukumbu. Napitisha ujumbe huu kwenye jukwaa la mabadiliko lakini narithia kwamba chombo chochote cha habari kinanaweza kuuchapisha, nimeridhia.
 Nauona  ujumbe huu kama ujumbe wa mtu aliyae nyikani . Hivyo kwa  heshima na taadhima nakuomba  Rais wangu uusome na kuutafakari  kwa jinsi Mungu anavyokujalia.
Rais wangu Kikwete, awali ya yote niweke bayana kwako kwamba mimi Ananilea Nkya, sina chama chochote cha siasa ninachofungamana nacho na wala sina mpango wowote wa kuwa mwanasiasa ama kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kisiasa.  Naridhika sana na taaluma yangu, na hakika nijuavyo mimi, mwanahabari  anayetambua  na kutekeleza majukumu yake kwa taifa lake, mchango wake unakuwa ni    mkubwa pengine kuliko  mchango wa mtu mwingine yeyote  katika nchi yake.
Rais  wangu, ujumbe wangu ni mfupi tu, kwamba tulipofika sasa kama nchi,  hakuna Rais awe  kupitia Chadema, CCM,  NCCR Mageuzi au chama kingine chochote atakayeweza kuivusha nchi hii 2015 kwa hali tuliyofikia sasa.   Mwanasiasa pekee mwenye UWEZO na MAMLAKA  wa  kuivusha nchi hii tuweze kubaki  salama kama taifa moja la watu wanaopendana kwa dhati ni wewe peke yako.
 Rais wangu Kikwete, kwa maono niliyoyapata usiku wa kuamkia leo,  nakuona ukiivusha nchi yetu hii  kwa kujitoa mhanga ipatikane KATIBA MPYA YA UKWELI itakayondoa mamlaka   mikononi mwa mtu mmoja mmoja au chama kimoja kimoja na badala yake  kurejesha mamlaka mikonomi mwa umma wa  Watanzania, ili tuepuke balaa la umwagaji damu linaloinyemelea nchi yetu  tuendako.
Rais wangu Kikwete, mimi ni ndugu yako wa ukweli. Ni Mtanzania ninayeipenda na kuithamini sana nchi yangu na wananchi wenzangu. Nakuomba ufungue macho yako ya rohoni uione TUZO YA DUNIA YA UTUMISHI ULIOTUKUKA inayokuja taratibu kwako  kutokana na utumishi wako ukiwa Rais wetu.
 Lakini Rais wangu Kikwete, ukiwasikiliza wasioithamini Tanzania na roho za Watanzania wenzao, watu wenye fikra kwamba chama cha siasa ni zaidi ya nchi  na kufanya mambo yanayotoa dhana kwamba  CCM  ni zaidi  ya Tanzania,  na kwamba bila CCM kutawala hakuna Tanzania,  nishani hiyo itakuponyoka, na hakika mimi  nitasikitika sana.
Rais wangu  Kikwete, nakutia shime, songa mbele kwa UJASIRI upate kuifikia na kuipokea  nishani yako, Tanzania  tujulikane duniani kote na heshima yetu ipande juu  kama nchi ya mfano inayoweza kufanya mabadiliko yake ya ukweli kwa amani, furaha na mshikamano. Siku hiyo ya wewe   utakapokuwa unapokea  nishani hiyo, Mimi Ananilea Nkya, ni mmoja wa Watanzania  watakaobubujikwa na machozi ya furaha  kwa kuifikisha TANZANIA kwenye USHINDI.
Binafsi Rais wangu Kikwete, ninakuamini na kukuthamini sana maana ninakujua toka zama ukishiriki nasi harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi pale kwenye matamasha ya jinsia ambayo  yalikuwa yanaandaliwa kwa pamoja kati ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na mashirika washirika wa FEMACT  Nakujua ualisia wako unapoamua kusimamia jambo, linatoka.
Mungu akubariki sana  na aendelee kukutunzana, na sote tuendelee kuombeana. Mimi kwa sasa niko masomoni ninaamini Mungu akitutajilia tutaonana siku hiyo ya TUZO au kwenye harakati ukistaafu.
Wasalaam,

Leave your comment about RAIS KIKWETE JIANDAE KISAIKOLOJIA KUPOKEA TUZO YA DUNIA using the comment form below

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here