Taarifa ya Dk. Kitila Mkumbo Kuhusu Kuvuliwa Uongozi Ndani ya CHADEMA

0
655
Taarifa ya Dk Kitila Mkumbo kwa Vyombo vya Habari

Taarifa ya Dk. Kitila Mkumbo kwa Umma kuhusu Kuvuliwa nafasi za mamlaka
ndani ya CHADEMA

1. Katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika tarehe 20-22
Novemba 2013, pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa waraka wa siri
unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013. Waraka huu ulilenga kujenga
hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuanisha mikakati ya ushindi kwa
mgombea mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya CHADEMA. Nilikiri kuwa
nilikuwa naufahamu waraka huu, na kwamba nilishiriki kuuandaa na kuuhariri, na
kwamba mimi ni mmoja wa wanachama wanaoamini kwamba kuna haja ya
kubadilisha uongozi wa juu wa chama katika uchaguzi ujao ndani ya chama.

2. Katika mjadala, maudhui ya waraka huu yalionekana kwa wajumbe kwamba
yalikuwa na mapungufu na yalikiuka misingi na kanuni zilizoanishwa katika
Katiba ya Chama. Kwa kuwa katika chama cha siasa hoja za watu wengi ndizo
hupewa uzito, na kwa kuwa dhamira na nia yangu ndani ya chama hiki imekuwa
ni kusukuma mabadiliko ambayo watanzania wanayatazamia nje ya mfumo wa
sasa wa utawala, nilikiri makosa yangu na kuwaomba msamaha wajumbe wa
Kamati Kuu na viongozi wakuu wa chama, na kueleza kwamba nilikuwa tayari
kujiuzulu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Wajumbe walikataa
kukubali ombi langu la kujizulu bali walipitisha azimio la kunivua mimi na Mhe.
Zitto Zuberi Kabwe nafasi zetu za uongozi. Nilipokea kwa unyenyekevu adhabu
ya kuvuliwa nafasi zote za mamlaka nilizokuwa nazo ndani ya chama hiki na
kueleza kuwa nitaendelea kutoa mchango wangu kama mwanachama wa kawaida
hadi hapo chama kitakapoona ninafaa kukitumikia katika nafasi yeyote.

3. Kufuatia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba
2013 ambapo, pamoja na mambo mengine, ilielezwa na viongozi wa CHADEMA
kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na Zitto Kabwe) tumehujumu
chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi kwa mgombea
tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo:

a. Siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya
chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa CHADEMA
ni demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa demokrasia
zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa
juu kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani
katika chama chetu.

b. Sijawahi na sitarajii kushiriki vitendo vyovyote vya kuhujumu chama
changu cha CHADEMA na harakati za mabadiliko hapa nchini. Chama
hiki kiliniamini katika nafasi nyingi nyeti sana na kama mie ningekuwa
mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo. Nimeshiriki
kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010
nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa Baregu na
nilishiriki kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata wabunge
wa viti maalumu katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti mno ambazo
kamwe huwezi kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’.
Nilishiriki katika shughuli za chama kwa kiwango ambacho
nilijisababishia matatizo makubwa katika familia yangu na kazini, lakini
sijawahi kutetereka na sijaterereka. Nilifanya yote haya kwa mapenzi
yangu ya dhati na imani yangu kwa CHADEMA kwamba ndicho chama
kinachostahili kuongoza harakati za mabadiliko hapa nchini kwa sasa.

c. Nasikitika kwamba nimesababisha usumbufu kwa viongozi wangu wa
CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka mabadiliko ya uongozi
ndani ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia. Nilifanya hivi kwa
imani niliyo nayo kwa misingi ambayo CHADEMA inasimamia, ikiwemo
demokrasia, na imani yangu kwamba chama hiki kinahitaji kufanya
mabadiliko makubwa katika uongozi wa juu wa chama, ikiwa ni
maandalizi muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Nasisitiza
tena kwamba siamini hata kidogo kwamba matamanio ya mabadiliko ya
uongozi ndani ya chama, na kuandaa mikakati ya kufikia matamanio
hayo kwa njia za kidemokrasia ni uhaini.

d. Tunaweza kujifunza kutokana na historia. Siasa za ushindani ndani ya
vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi za TAA na kabla TANU
haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za uongozi mezani.
Lakini mwaka TANU ilipozaliwa (mwaka 1954) kulikuwa na uchaguzi
mkali sana kwa nafasi ya uenyekiti. Mwalimu Nyerere alimshinda Mzee
Skyes kwa kura chache sana. Rais Obama wa Marekani alianza mkakati
wa kushinda uteuzi wa kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake cha
Democrat mapema kabisa mwaka 2006 kupitia waraka maalumu wa siri
ulioainisha mikakati yake. Waraka huu uliandaliwa na watu wanne tu bila
yeye mwenyewe kujua. Waandaji wa mkakati huu walikuja kumshirikisha
baadaye mwaka 2007 na kumshawishi yeye ajitokeze kugombea dhidi ya
Hillary Clinton aliyekuwa anachukuliwa kama mrithi halali wa kiti cha
urais. Yaliyobaki ni historia. Hivi ndivyo ambavyo siasa za ushindani
ndani ya vyama hatimaye huzaa wagombea na viongozi imara katika nchi.

e. Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa sababu ya waraka huu kwa sababu
yeye hakuhusika kwa namna yeyote kuandaa, ingawa alikuwa ni mlengwa
mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye atazieleza na ambazo
viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na waandishi wa
habari.

f. Napenda ijulikane kwamba sikuomba kujiuzulu kwa sababu ya kuogopa
aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa sababu nilitambua kwamba
wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami tena, na ni
uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile
kwamba, kwa mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo
wa kunivua nafasi yangu moja kwa moja. Kwa mujibu wa Katiba ya
CHADEMA, Sura ya Sita, Ibara ya 6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi
aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa
uongozi na kikao kilichomteua”. Mimi nilichaguliwa na Baraza Kuu na ni
kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua nafasi niliyokuwa nayo.
Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu walipitiwa katika hili kwa sababu
siamini kwamba hawajui takwa hili la kikatiba ukizingatia kwamba ndani
yake kuna wajumbe waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria.

4. Hiki kilichotokea ndani ya chama sio kitu kibaya. Vyama vingi imara hupitia
katika migogoro na misukosuko kama hii na zaidi. Naamini tutavuka na tutakuwa
imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima tuaminiane. Katika kuaminiana sio
lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa sababu hili ni jambo
lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa.

5. Ninapohitimisha, ninawasihi wanachama wa CHADEMA na wapenzi wa
mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati MISINGI mama ya CHADEMA
ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo chama chochote
kinaweza kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika nchi wakati
kinayahainisha mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe.
Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu demokrasia na ni
usaliti kwa misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa kweli na mabadiliko
ya kweli. Hisia za usaliti na umamluki zilitumika enzi za ukomunisti katika
kunyamazisha wapinzani ndani ya vyama vya siasa na katika nchi. Zilikuwa ni
njia haramu zilizozoeleka ambazo hatimaye zilizaa udikteta wa kutisha katika
mataifa ya kikomunisti. Tusikubali utamaduni wa kuhisiana usaliti na umamluki
ukaota mizizi katika chama chetu na katika nchi kwa sababu utaua demokrasia na
mfumo wa vyama vingi utakuwa hauna maana tena.

6. Nitafuata taratibu zote za chama kama zilivyoelekezwa na Kamati Kuu na kwa
mujibu wa katiba yetu, na nitashiriki kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa
ndani ya chama ili kuhakikisha kwamba tunabaki imara, na CHADEMA
inaendelea kuwa tumaini la watanzania.

Mungu ibariki Tanzania.

Dkt. Kitila Mkumbo
Dar es Salaam
Jumapili, 24 Novemba 2013.

Leave your comment about Taarifa ya Dk. Kitila Mkumbo Kuhusu Kuvuliwa Uongozi Ndani ya CHADEMA using the comment form below

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here