Utapeli kwa Njia ya simu

0
358

Jumamosi wiki hii nikiwa kazini, nilipokea ujumbe ufuatao kutoka namba 0714-530869 ulioambatana na mneno yafuatayo “Habari za kazi ndg yangu Kulwa, mm Charles Mganga, simu yangu ina matatizo kdg, upo wapi muda huu? naomba unijib kwa msg niko kikaoni“. Baada ya kupokea ujumbe huo na kwa kuwa huyo Charles Mganga nafanya naye kazi, niliamua kuujibu ujumbe hata kabla sijaangalia ofisini kujua kama Mganga mwenyewe alikuwepo au la, nikajibu “Niko ofisini, unasemaje?” Kisha namba hiyo hiyo ikatuma ujumbe mwingine unaosema ” Ok, samahani naomba nikupe namba ya mjomba wangu unisaidie kumtumia elf 30, nikimaliza kikao nitakupa” Bahati nzuri wakati napokea ujumbe huo nilikuwa na mfanyakazi mwenzangu jirani ambapo nilianza kumlalamikia kuhusu ujumbe ule wa awali nikidai kuwa huyu Mganga mbona ananituma ujumbe wa kunitaka nimtumie fedha nduguye bila kujua kama pesa hizi ninazo au la. Palepale yule mfanyakazi mwenzangu alinijibu mbona Mganga yuko ofisini kwake! Kilichofuata nilimfuata Mganga na kumuuliza kulikoni anitumie ujumbe ilhali yuko ofisini na tena anidanganye kuwa yuko kikaoni wakati anawajibika kwa mwajiri ndani ya ofisi. Yule bwana alishangaa sana na kusisitiza kuwa hajaandika ujumbe na wala haijui namba iliyonitumia ujumbe.
Wakati tunaongea-tukakubaliana tuipige namba hiyo ili tumsikilize vizuri mtu anayejiita Mganga, ambapo simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa. Mwisho wa siku alituma tena ujumbe akisema “Naomba unitimie sms ndg yangu niko kikaoni”
Palepale tukavuta hisia na jamaa zangu wale ofisini ambapo miezi kadhaa iliyopita, namba hiyo hiyo iliwahi kutumiwa kutapeli waandishi na wahariri fulani wa vyombo vya habari na hata sisi kwa utatu wetu (tuliokuwa pamoja ofisini Jumamosi) iliwahi kututapeli namba hiyo, lakini hatukuuingia mkenge huo na taarifa kuhusu namba na mhusika tulifikisha katika kituo cha polisi cha Msimbazi ili zifanyiwe kazi. Kinachoonekana ni kuwa mmiliki wa namba hiyo ambaye uchunguzi wetu wa awali baada ya tukio la kwanza, ni mwanamke maana kumjjua mtumiaji wa namba ya simu siku hizi ni rahisi, iwapo unaweza kumtumia tu hata kama ni sh. 200 kwa mtandao wowote jina lake litakuja katika meseji utakayojibiwa. Polisi waliahidi kuwa watafuatilia na mhusika atafikishwa mbele ya vyombo vya dola.
Wadau nimeileta kwenu namba hii ili muwe makini. Nchi yetu kwa sasa imegubikwa na wizi wa kutisha wa mitandao, kuanzia ile ya mawasiliano ya kompyuta hadi simu ingawa wanaotapeliwa wengi hawasemi tu.

Leave your comment about Utapeli kwa Njia ya simu using the comment form below

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here