Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi za Serikali Kuharibu Uchaguzi

0
721

SIKU TANO ZA KAMPENI: YAFUATAYO YANAONESHA DHAHIRI KUWA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA NA MAMLAKA ZA SERIKALI ZINASHIRIKIANA NA CCM KUJARIBU KUHARIBU UCHAGUZI HUU;

Na. Julius Mtatiro.

1. Kumzuia mgombea urais wa CHADEMA/UKAWA kuhudhuria msibani eti kwa sababu amesindikizwa na watu, kana kwamba watu walewale kwa idadi ileile wangekwenda wenyewe wangeleta madhara yoyote. Najiuliza tu, ingekuwaje mgombea na watu wale wangelazimisha kwenda msibani; JIBU: Mapambano na Polisi, mgombea kukamatwa na kufunguliwa kesi, wafuasi kujeruhiwa kwa risasi, kuuawa ama kukamatwa.

2. Kupiga Marufuku maandamano na mbwembwe za kuwasindikiza wagombea kurejesha fomu. Hili lilifanywa mara baada ya Magufuli na Lowassa kwenda kwa maandamano lakini yale ya Lowassa yakionekana kuwa na maelfu mengi ya watu zaidi kuliko ya magufuli. Lakini pamoja na marufuku hiyo majuzi nimejionea wafuasi wa CCM wakiandamana kutoka Manzese hadi Jangwani wakiwa na MASABURI, bila polisi kuwazuia.

3. Kuzuia mgombea wa UKAWA/CHADEMA kufanya ziara maalum za kushtukiza kuwatembelea wananchi wa kawaida. Hizi zinapigwa marufuku kwa mgombea huyu wakati wale wa CCM wakifanya watakavyo. Mfano ni Bi. Samia Suluhu alivyoonekana Moshi akiacha ratiba ya ziara na kutembelea raia mtaani bila kukatazwa na Polisi. 

4. Kuzuia UKAWA kufanya mkutano wake wa uzinduzi Uwanja wa Taifa na hata UKAWA ilipoamua kufanyia mkutano huo katika viwanja wa JANGWANI umezuiwa na Manispaa ya Ilala nadhani kwa shinikizo la CCM chini ya sababu dhaifu sana kwamba kuna watu wameshaukodi, Ni halmshauri ipi hivi sasa ambayo ina-PRIORITIZE shughuli zingine kwenye viwanja vikubwa wakati vyama vya siasa viko kwenye uchaguzi mkuu jambo ambalo ni kipaumbele cha taifa kwa sasa?

5. CCM kufanya mkutano wake wa uzinduzi hadi saa 12.38 jioni tena mbele ya Mkuu wa nchi na viongozi wote wa serikali wakati wanajua fika kuwa sheria inawataka kufunga mkutano saa 12.00 jioni. Kwamba CCM na inavionesha vyama vingine kuwa iko juu ya sheria na kwamba wengine wakiiga watajiju. Na baada ya kupitisha muda huo CCM inamshinikiza Mkurugenzi wa manispaa ya ILALA aandike barua NEC kuijulisha kuwa ni yeye ndiye alielekeza mkutano uendelee hadi muda huo (very illogical reason).

6. Rais mstaafu wa awamu ya 3 Benjamin William Mkapa kusimama hadharani na kuwatukana wapinzani kuwa ni “MALOFA na WAPUMBAFU”. Mpumbavu ni neno kali na lina maana ya “juha”, “zuzu”, “mtu asiyejielewa”, “—–“, “—-“, n.k. Wakati Mkapa akitukana hivyo hadharani na kuachwa juu ya Sheria, Lawrence Masha ambaye ni mwana UKAWA (hivi sasa) lakini zamani akiwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Tanzania, yeye amekamatwa na kuwekwa rumande na kunyimwa dhamana (inacheleweshwa kimakusudi) kwa “kosa” la kumtukana askari polisi (wengi kama sikosei) kwamba ni “washenzi”, “wasio na shukrani na wasio na dini”. Kwamba kwa tafsiri ya CCM na serikali yake pamoja na vyombo vinavyosimamia sheria (POLISI), neno “Upumbavu na Ulofa” siyo tusi lakini neno “Ushenzi na Kutokuwa na shukrani” ni tusi baya sana.

Hayo mambo sita niliyoyataja na mengine kadhaa ni dalili tosha kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaweza kuishia mahali pabaya. Hadi sasa sijaona CHOKOCHOKO kutoka upande wa UKAWA, hii ina maana kwamba hizi za CCM, VYOMBO VYA DOLA NA MAMLAKA ZA SERIKALI zikiendelea na zikawa zinahujumu kwa dhahiri maslahi ya UPINZANI na UKAWA, lolote lile linaweza kutokea.

Julius Sunday Mtatiro,
Dar Es Salaam.

Leave your comment about Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Taasisi za Serikali Kuharibu Uchaguzi using the comment form below

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here